Rais Samia atoa Bilioni 40 kutekeleza miradi ya elimu Ruvuma

0
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas.

Na Albano Midelo, Songea

RAIS Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa Shilingi Bilioni 40 kwa ajili ya kutekelezaji miradi mbalimbali katika sekta ya elimu mkoani Ruvuma.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas wakati anatoa taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi Mkuu wa CCM kwa kipindi cha Julai hadi Desemba 2022 na Januari hadi Juni 2023 kwenye ukumbi wa Parokia ya Bombambili mjini Songea.

Akizungumzia sekta ya elimu Kanali Thomas alisema, katika kipindi hicho sekta ya elimu ilipokea Shilingi Bilioni 7.7 kujenga shule mpya za sekondari katika Halmashauri zote nane zilizopo mkoani Ruvuma

“Ujenzi huu unajumuisha shule za sekondari za kata kumi zilizogharimu Shilingi Bilioni 4.7,shule ya sekondari mpya ya wasichana ya Mkoa iliyopewa jina la Dkt. Samia Suluhu Hassan iliyojengwa wilayani Namtumbo kwa gharama ya Shilingi Bilioni 4.1’’,alisema.

Aliongeza, sekta ya elimu pia ilipokea fedha za ujenzi wa mabweni saba ya wanafunzi wa shule za msingi na sekondari kwa gharama ya Shilingi Milioni 640 na ujenzi wa vyumba vya madarasa 792 vya elimu ya msingi na sekondari vilivyogharimu Shilingi Bilioni 14.93.

Jengo la utawala katika shule mpya ya sekondari Luhira Manispaa ya Songea ambapo serikali imetoa shilingi milioni 470 kupitia program ya SEQUP ambapo katika Mkoa wa Ruvuma kupitia programu ya SEQUIP serikali imetoa Shilingi Bilioni 7.7 kujenga shule mpya za sekondari.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa, Rais Samia pia katika sekta ya elimu ametoa Shilingi Milioni 250 kujenga shule mpya ya msingi katika kitongoji cha Lizaboni Halmashauri ya wilaya ya Songea.

Aidha, Serikali imetoa fedha zaidi ya Shilingi Bilioni Mbili kukamilisha vyumba vya madarasa 121 vya shule za msingi na sekondari Pamoja na maabara 23 za shule za sekondari kupitia fedha za Tozo na Serikali Kuu.

Kulingana na Mkuu wa Mkoa, katika sekta ya elimu Rais Samia pia ametoa Shilingi Bilioni 3.12 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba 156 vya madarasa katika shule za sekondari mkoani Ruvuma hali iliyosababisha kuondoa kabisa tatizo la upungufu wa vyumba vya madarasa.

Mkuu wa Mkoa aliongeza kuwa, walimu wote wa shule za msingi na sekondari wapatao 9,079 katika Mkoa wa Ruvuma wamegawiwa vishikwambi kwa ajili ya uboreshaji wa ufundishaji. Mkoa wa Ruvuma una jumla ya shule za msingi 841 na shule za sekondari 233.

Majengo ya utawala na baadhi ya vyumba vya madarasa katika shule ya sekondari ya wasichana Mkoa wa Ruvuma iliyojengwa wilaya ya Namtumbo na kupewa jina la Dkt. Samia Suluhu Hassan ambapo serikali imetoa Shilingi Bilioni 4.1 kutekeleza mradi wa ujenzi wa shule hiyo  yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi zaidi ya 1000 wa kidato cha kwanza hadi cha sita. Tayari shule hiyo imeanza kuchukua wanafunzi wa kidato cha Tano kuanzia mwaka huu

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here