Tanzania na China kushirikiana kuboresha usafiri wa reli nchini

0
Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Prof. Godius Kahyarara akisaini Mkataba wa Utendaji kazi kwa Mwaka 2023/24 na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) Masanja Kadogosa (kushoto waliokaa), jijini Dodoma 2/10/2023. Kulia ni Mkurugenzi wa Kitengo cha Ufuatiliaji na Tathmini wa WIzara ya Uchukuzi, Devotha Gabriel.

Na Mwandishi Wetu

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi Prof. Godius Kahyrara amesema, Serikali ya Jamhuri ya Tanzania kwa kushirikiana Serikali ya China inatarajia kuliboresha Shirika la Reli la Tanzania na Zambia (TAZARA) ili kuliwezesha kuongeza ufanisi hususani katika usafirishaji wa mizigo.

Prof. Kahyrara ameyasema hayo jijini Dodoma wakati aliposaini mkataba wa Utendaji kazi na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) na kusisitiza kuwa tija ya maboresho hayo ni pamoja na kukuza pato pato la Taifa na urahisi kwenye usafirishaji wa mzigo kutoka eneo moja kwenda jingine.

“Shirika la TAZARA ni moja ya Mashirika ambayo yanapewa kipaumbele kwa sasa hasa katika uboreshaji wa miundombinu ambayo kwa muda mrefu haikukarabatiwa na wenzetu wa Serikali ya China wameonyesha nia ya kusaidia kwenye eneo hilo,” alisema Prof. Kahyrara.

Katibu Mkuu Prof. Kahyrara amesema tayari Serikali imefanya maboresho katika Sheria ya Reli ili kuruhusu sekta binafsi kutoa huduma katika Reli ya TAZARA na TRC.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa TRC Masanja Kadogosa alisema, miradi mbalimbali inaendelea kutekelezwa kwa reli ya Kati na Reli ya Kisasa ambayo hivi karibuni majaribio yatafanywa na kuanza kutoa huduma.

Mkurugenzi Kadogosa aliongeza kuwa, vitendea kazi kwa ajili ya uendeshaji wa SGR vimeendelea kuwasili, ambapo hivi karibuni TRC imepokea Kichwa kimoja cha reli hiyo kutoka Korea Kusini; kichwa hicho ni miongoni mwa vichwa 17 ambavyo vimeagizwa.

Naye Mkurugenzi wa Tathimini na Ufutiliaji kutoka Wizara ya Uchukuzi Devota Gabriel amemuhakikishia Katibu Mkuu Prof. Kahyarara kuwa kitengo hicho kimewekea mikakati thabiti itakayowezesha wataalam wa Wizara kusimamia kwa karibu miradi iliyopangwa kutekelezwa kwa mwaka wa fedha 2023/2024 ili kuzingatia thamani na ubora.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here