Na Mwandishi Wetu
KATIBU Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Daniel Chongolo amewataka Watanzania kushirikiana kulinda miundombinu ya Reli ya Kisasa ya SGR, akisema Serikali mpaka sasa imetumia kiasi kikubwa cha Fedha ili mradi huo ukamilike kwa wakati.
Katibu Mkuu Chongolo amebainisha hayo Wilayani Kilosa alipofika kukagua hatua za Ujenzi wa mradi huo, ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya Kikazi Mkoani Morogoro yenye lengo la Kukagua Utelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025.
Alisema, ni lazima kwa Wananchi kutambua thamani halisi ya Fedha zilizotumika kwenye Ujenzi wa mradi huo wa Reli ya Kisasa ya SGR kuwa ni kwa ajili ya manufaa ya Watanzania wote, kwa hiyo ni muhimu kuilinda miundombinu hiyo ya Reli.
“Hakuna mtu aliyejenga kwa Fahari yake Binafsi, kwani hii Stesheni itakuja kutumiwa na Rais?… hata akija atatumia siku moja tu, watakaonufaika ni Watanzania wote, hata ukiona huwezi kuja kupiga picha hapa?..Lazima tulinde miundombinu hii kwa Sababu tija yake ni kubwa” amesema Chongolo.
Awali, Mkurugenzi mkuu wa TRC, Masanja Kadogosa akiwasilisha taarifa ya Ujenzi wa mradi huo wa Reli ya Kisasa SGR, amemhakikishia Katibu Mkuu huyo wa CCM, kuwa Reli hiyo itaanza kufanya Safari zake Ifikapo Mwezi April mwaka huu kama Changamoto zilizojitokeza awali zitakuwa zimetatuliwa ikiwemo ya kuwasili kwa Vichwa vya treni hiyo.
Katibu Mkuu Chongolo yupo kwenye ziara ya kusimamia, kukagua na kuhimiza utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya mwaka 2020-2025 akiwa ameongozana na Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi Ndugu Sophia Mjema, Katibu wa NEC Oganaizesheni Ndugu Issa Ussi (Gavu), pamoja na viongozi wengine wa Chama na Serikali kutoka mkoani humo na Wilaya ya Kilosa.