Na Mwandishi Wetu
HOSPITALI ya Taifa Muhimbili – Mloganzila imezindua huduma mpya ya kuweka puto maalumu kwenye tumbo la chakula kwa watu wenye uzito uliopitiliza (intragastic ballon) ambayo itasaidia kupunguza nafasi kwenye tumbo la chakula hivyo kusababisha mtu kula kidogo jambo ambalo litapelekea kupungua uzito.
Akizindua huduma hiyo leo Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof. Mohamed Janabi alisema, Mloganzila ndio Hospitali ya kwanza ya umma Tanzania kutoa huduma hiyo hivyo amewapongeza wataalamu kwa kufanikisha jambo hilo.
“Hadi leo tumefanya kwa watu 3 na kuna zaidi ya watu 12 ambao wanahitaji huduma hiyo, wanaotakiwa kupatiwa huduma hii ni wale wenye uzito uliopitiliza ambao ni kuanzia kilo 100,” alisema Dkt. Janabi.
Kuhusu gharama za huduma hiyo , Prof. Janabi alifafanua kwamba, kwa Mloganzila inagharimu Shilingi Milioni 3.5 hadi Shilingi Milioni 4, wakati nje ya nchi ni zaidi ya Shilingi Milioni 15.
Kwa upande wake Daktari Bingwa wa Upasuaji, Dkt. Eric Muhumba alisema, huduma ya kuweka puto hufanyika kwa dakika 20 ambapo hufanyika kwa kutumia mashine ya Endoscopia (Endoscopy Mashine) hivyo haihusishi upasuaji wa aina yoyote.
Dkt. Eric aliongeza kuwa, puto likishawekwa tumboni hukaa kwa muda kati ya miezi sita hadi nane ndipo hutolewa na baada ya hapo mtu huyo atakuwa ameshajenga utamaduni wa kula kidogo hivyo atakuwa amepuguza uzito wa kutosha.
Pia, Dkt. Eric ameishauri jamii kufanya mazoezi na kula chakula kwa kuzingatia ushauri wa wataalamu wa lishe ili kuwa na afya bora na kuepuka kupata uzito uliopitiliza ambao unasababisha magonjwa mbalimbali ikiwemo kisukari, magonjwa ya moyo na kiharusi.
Naye, Mjumbe wa Kamati ya Utalii Tiba (Medical Tourism) AbdulMarik Mollel ameipongeza MNH-Mloganzila kwa kuzindua huduma hiyo ambayo itafungua milango kwa watu kutoka nchi jirani kuifuata kwa kuwa ni salama na gharama zake ni nafuu hivyo kusaidia kuitangaza Tanzania.