Rais Samia apongezwa kwa jitihada za kuimarisha demokrasia nchini

0

Na Jumbe Abdallah

KIKAO cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa kilichokutana leo, kimempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa hatua ya kupokea ripoti ya kikosi kazi alichokiunda kuratibu maoni na mapendekezo ya wadau mbalimbali juu ya mchakato wa mustakabali wa Taifa katika uendeshaji wa siasa.

Taarifa iliyotolewa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa, Shaka Hamdu Shaka ilisema kwamba, tangu alipoingia madarakani, Rais Samia ambaye amekuwa mstari wa mbele katika kusimamia utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM 2020-2025, kuimarisha demokrasia ya vyama vingi vya siasa nchini na ujenzi wa maridhiano ya kitaifa.

Shaka alisema, Rais Samia ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM, amechukua hatua hizo ili kuliwezesha taifa kuendelea kuwa lenye utulivu wa kisiasa, umoja na amani kwa maendeleo endelevu.

Aidha, Kamati Kuu imempongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa hatua yake ya kuendelea kuimarisha mahusiano ya kisiasa visiwani Zanzibar ambapo ameunda kikosi kazi cha kuratibu maoni kwa upande wa mambo maalum yanayohusu Zanzibar na kinaendelea vyema na majukumu yake hatua ambayo itaimarisha demokrasia, umoja na mshikamano.

Katika hatua nyingine Kamati Kuu imepokea taarifa ya awali ya maandalizi ya Mkutano Mkuu wa kumi (10) wa CCM Taifa unaotarajiwa kufanyika mwezi Disemba, 2022. Kamati Kuu imeridhishwa na hatua mbalimbali za maandalizi ya Mkutano Mkuu huo wa kawaida utakaofanyika kwa mujibu wa Katiba ya CCM ya mwaka 1977 toleo la mwaka 2022 Ibara ya 99(3),

“Mkutano Mkuu wa CCM wa Taifa utafanya mikutano yake ya kawaida mara tatu katika kipindi cha miaka mitano. Mikutano miwili kati ya hiyo itakuwa ya uchaguzi na mmoja utakuwa wa kazi. Kalenda ya vikao vya chama itaonesha ni lini Mikutano mitatu hiyo itafanyika.”

“Lakini mkutano usiokuwa wa kawaida unaweza kufanyika wakati wowote ukiitishwa na Mwenyekiti wa CCM au ukiombwa na theluthi mbili ya wajumbe wote wa Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa.” alisema Shaka.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here