Kiwanda cha Mponde kuzalisha ajira na kuinua kipato cha wakulima

0

Na Mwandishi Wetu, Lushoto

MWENYEKITI wa Bodi ya Wadhamini wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), Mhandisi Musa Iyombe amesema, wameridhishwa na ukarabati uliofanyika kwenye kiwanda hicho ambacho kimeanza uzalishaji.

Mhandisi Iyombe alisema hayo mwishoni mwa wiki, akiwa na wajumbe wengine wa Bodi ya Wadhamini wa PSSSF waliotembelea kiwanda hicho kilichopo katika kijiji cha Kweminyasa, wilayani Lushoto ili kukagua maendeleo ya ukarabati wa kiwanda hicho.

“Tumetembelea kiwanda hiki cha Mponde ambacho kinazalisha chai bora, chai nzuri ambayo inaweza ikatumika ndani na nje ya nchi. Kiwanda kipo vizuri baada ya ukarabati, tumeona kiwanda kimeanza kuchakata majani ya chai, naamini wakulima wenye mashamba kwenye wilaya ya Lushoto, hususan Bumbuli, Korogwe na maeneo jirani watanufaika sana na uwepo wa kiwanda hiki” alisema Mwenyekiti wa Bodi ya PSSSF.

Mhandisi Iyombe alisema, kuanza uzalishaji kwa kiwanda cha Chai Mponde ni wazi kwamba vijana wengi watapata ajira na kwamba uchumi wa kata ya Mponde na wilaya ya Lushoto, ikiwemo Bumbuli na maeneo jirani utakuwa iwapo fursa ya kuwepo kwa kiwanda itatumiwa vyema.

Kwa upande wake, Meneja wa Kiwanda hicho, Sane Kwilabya alisema, “kwa upande wetu tumejipanga vyema kuzalisha chai bora katika kiwanda hiki, na tunaamini ardhi ya huku ni nzuri kwa kilimo cha majani ya chai yaliyo bora.”

Msimamizi wa ukarabati wa mradi huo, Mhandisi Ally Shanjirwa alisema ukarabati wa kiwanda hicho umekamilika kwa asilimia mia moja (100%) na sasa kinachofanyika ni kujaribu mitambo ili kubaini dosari na kuzirekebisha.

Kiwanda cha Chai Mponde kinaendeshwa kwa pamoja kati ya PSSSF na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) kupitia kampuni ya Mponde Holding Company Limited, ambapo kila Mfuko umewekeza asilimia 42 na Msajili wa hazina anamiliki hisa 16.

Kiwanda kinategemewa kuzalisha ajira za muda mrefu zisizopungua 79 na ajira za muda mfupi zinazokadiriwa kuwa kati ya 100 hadi 300 kutegemea na msimu wa mavuno ya majani ya chai.

Uwepo wa kiwanda cha Chai Mponde kitaongeza kipato kwa wakulima wa chai katika Halmashauri ya Bumbuli na maeneo jirani, kuongeza mapato kwa taifa kupitia kodi mbalimbali na kuongeza kipato cha fedha za kigeni kwa taifa kupita mauzo ya nje ya chai ya Mponde.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here