Serikali haina jambo dogo – Dkt. Abbasi

0

Na Adeladius Makwega – WUSM

SERIKALI imesema kuwa kufanyika kwa mashindano ya Urembo na Utanashati ya Viziwi ya Dunia nchini Tanzania Oktoba 29, 2022 ni heshima kubwa sana na Serikali haitokubali taifa letu kupata aibu yoyote ile machoni mwa mashindano haya, kwenye uso wa dunia na Serikali haina jambo dogo.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo nchini Dkt. Hassan Abbasi wakati akizungumza na kamati ya maandalizi ya mashindano hayo ya kitaifa Jijini Dar es Salaam Oktoba 17, 2022.

“Taifa na Serikali nzima tunatambua hilo na kama ilivyo falsafa ya Waziri wetu wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Mohamed Mchengerwa kwa sasa wizara hii haitokuwa na jambo dogo, hivyo ndivyo ilivyokuwa katika mashindano ya Urembo na Utanashati ya Viziwi ya Afrika na ndivyo itakavyokuwa katika mashindano haya ya Urembo na Utanashati ya Dunia.”

Tanzania imepata heshima kubwa na sasa nchi yetu imefunguka, tupo katika maandalizi ya mashindano haya, vinginevyo tungekuwa wapi ? Fursa hii inatumika kuitangaza nchi yetu, Watanzania tuchangamkie fursa zote, alisisitiza.

Dkt. Abbasi ameongeza kuwa, kila mmoja kwa nafasi yake ya ujumbe wa kamati hii ashiriki vizuri kutekeleza majukumu yake, kinyume chake hakuna Mtanzania anayekubali kupata aibu na huo ndiyo msimamo wa Serikali na kila maandalizi yafanyike kwa kiwango cha juu zaidi.

Katibu Mkuu Dkt. Abbas alimalizia kwa kusema, “Utalii si kutazama wanyama, kila pahala duniani kuna wanyama, utalii ni hata namna ya kumpokea mgeni tangu anavyoingia hadi siku anapoondoka nchini Tanzania, jamani tuitumie fursa hii.”

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here