Na Mwandishi Wetu
DUNIANI tuna makundi mawili; viongozi na wafuasi. Mara nyingi wanaofanikiwa na kufikia malengo waliyojiwekea ni wale waliopo kwenye kundi la viongozi.
Viongozi huanzisha na wafuasi hufuata au kuiga, hii ndio inawafanya viongozi wanafanikiwa kwenye mipango yao. Hakuna mtu anayepanga huyu awe kiongozi na huyu awe mfuasi. Ni mfumo wako wa maisha na tabia zako zitakuweka kwenye kundi la viongozi au kundi la wafuasi.
Je, unajua wewe upo kwenye kundi gani? Unaweza kujiita kiongozi kwa kuwa umepewa nafasi ya kuwasimamia watu, ila kama hauna sifa za uongozi basi wewe sio kiongozi, bali ni msimamizi tu.
Hapa tutaangalia tofauti tano za kitabia kati ya viongozi na wafuasi. Kwa kuzijua tofauti hizi za kitabia itakufanya ujue upo kundi gani na pia uweze kuchukua hatua.
- Uanzilishi.
Viongozi huanzisha mambo kutokana na malengo na mipango yao kwenye maisha na kazi wanazofanya. Hujua ni nini watafanya kwenye kila hatua na mwishowe hufanikiwa.
Wafuasi hufanya mambo yaliyoanzishwa na watu wengine. Hata siku moja hawana udhubutu wa kuanzisha kitu chao wenyewe na kukisimamia mpaka kitoe majibu wanayotarajia. Wafuasi huishia kuiga mambo yanayofanywa na watu wengine na inakuwa rahisi kwao kushindwa.
- Mawasiliano.
Viongozi huanzisha mawasiliano na watu wengine. Mara nyingi huwa wa kwanza kuwatafuta watu wanaowahitaji ili kukamilisha jambo fulani. Pia huwa wa kwanza kuwapigia wengine simu katika kuwasiliana.
Wafuasi huwa ni wasikilizaji kwenye mawasiliano. Ni wazuri wa kupokea taarifa walizopewa na kwenda kuzifanyia kazi. Kama wasipotafutwa hawajisumbui kutafuta mtu, hukaa na kusubiri. Wafuasi husubiri simu iite wapewe taarifa au maagizo.
- Matumizi ya muda.
Viongozi hutumia sehemu kubwa ya muda wao kupanga mipango mbalimbali. Pia hutumia muda huo kufikiria matatizo yanayoweza kutokea na kufikiria njia za kukabiliana nayo. Kwa njia hii viongozi wanaongeza uwezo wao wa kutatua matatizo.
- Uwekezaji wa muda.
Wafuasi hutumia muda wao mwingi kuishi maisha yao ya kawaida na hawana muda mwingi wa kuweka mipango mikubwa. Wafuasi ni wazuri kustushwa pale tatizo linapotokea na huwa wa kwanza kusumbuliwa na tatizo hilo. Kibaya zaidi wanakuwa hawana uwezo wa kutatua tatizo hilo zaidi ya kupata msongo wa mawazo.
Viongozi huwekeza muda wao kwa watu wengine. Hutumia muda wao mwingi kujenga na kufundisha watu kuwa viongozi. Pia hutumia muda kuwapa wengine uwezo wa kuweka mipango na kutatua matatizo.
Wafuasi hawawekezi muda wao bali wanautumia na watu wengine. Wafuasi wanapokuwa na muda wa ziada huutumia kufanya mambo ambayo hayana msaada wowote kwao kimaisha au kikazi. Ni watumiaji wa muda hovyo.
- Upangaji wa ratiba.
Viongozi wanapanga ratiba zao kulingana na vipaumbele vyao. Hupanga ratiba kutokana na malengo na mipango yao na huweka mbele vipaumbele vyao.
Wafuasi hupanga ratiba zao kulingana na maombi na maagizo. Ratiba za wafuasi zimejaa vitu ambavyo ni maombi ya watu wengine au ni maagizo ya watu wengine. Hawawezi kuweka vipaumbele vyao wenyewe kwenye ratiba zao. Hizo ndio tofauti tano kati ya viongozi na wafuasi kitabia. Hakuna mtu anayekupangia tabia hizi bali unaziendeleza mwenyewe.
Kama kwa tabia hizo hapo chini unajiona upo upande wa wafuasi usife moyo. Kama tulivyosema, viongozi pia hutengenezwa, hivyo unaweza kujitengeneza kuwa kiongozi mzuri na ukafanikiwa kwenye mipango yako ya maisha.
Nakutakia kila la kheri kwenye harakati zako za maisha, kumbuka viongozi ndio wanaofanikiwa kwenye nyanja yoyote na wafuasi hubaki wasindikizaji.