Hizi ndio ngurumo za Kinana
Kigoma hadi Mwanza

0

Na Umar Mukhtar

MWANASIASA Mkongwe Kanali Mstaafu Abdulrahman Kinana kwa takriban siku tano sauti yake imekuwa ikinguruma kwenye anga la mikoa ya Kigoma, Kagera, Geita hadi Mwanza .

Vyombo vya habari yakiwemo magazeti, luninga, radio na mitandao ya kijamii imekuwa ikiripoti kila uchao kuhusu ziara hiyo iliyokuwa na panda shuka ya milima na mabonde.

Kinana amekuwa katika fatiki kubwa ya uzinduzi wa miradi ya maendeleo ya kisekta ikiwemo kuendelea kwa ujenzi wa hospitali za wilaya, hospitali za Rufaa, zahanati na vituo vya afya.

Hakuacha kukutana na wanachama wa chama wa CCM katika mikutano ya ndani, akitoa misimamo na maelekezo ya chama inayoqataka wanaCCM kushikamana, kujenga upendo na kupendana wakati wote .

Hatari ya udini, ukabila na ukanda

Mara kadhaa Kinana katika vikao vya ndani na wanachama amekemea vikali vitendo vya rushwa, upendeleo, kubebana huku akilaani matumizi ya misamiati ya ukabila, udini na ukanda.

Hakusita kutaja hatari ya ukabila, udini na ukanda na kujikuta akikagua mbaraka akisema kinagaubaga ya kuwa mwanasiasa yeyote anayejiegemeza katika mambo ukabila na udini asichaguliwe na kuwa kiongozi wa CCM.

Makamu huyo Mwenyekiti wa CCM Bara amewakumbusha wanachama wake wosia wa marehemu Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere aliotoa wakati akiyakemeea majanga hayo mwaka 1995.

Mwalimu Nyerere akizungumza kwa hisia kali akawataka mashabiki wa ukabila, ukanda na udini kila wakati waogopwe kama ugonjwa wa ukoma.

Akasema majigambo ya kutumia ukabila, udini au ukanda yameyagawa Mataifa kadhaa ulimwenguni. Watu wasio hatia wakafikia wakamwaga damu na hata kuzuka vita ya wenyewe kwa wenyewe.

Siasa za ukabila na udini zimepoteza maisha ya wengu, zimejenga hasama na kuleta mipasuko ilioyaacha alama za nyufa zisizozibikana sasa Mataifa hayo yamebaki katika mgawanyiko na majuto.

Kadhalika Mwanasiasa huyo anayeheshimika katika siasa za Tanzania, Afrika Mashariki, Afrika na sehemu kubwa ya dunia, amelaumu mtindo uliochomoza ndani ya CCM kuhusu mwanachama kujiunga na chama asubuhi jioni anachukua fomu na kuwania uongozi.

Akasema, utamaduni huo si wa CCM kwani upo muda uliowekwa kwa mujibu wa Katiba na kanuni za CCM unaomtaka mwanachama huyo mpya kusubiri kwa kipindi fulani ndipo aweze kugombea.

Aidha, mwanachama mpya atalazimika kusubiri ili kuipitia na kuisoma katiba aweze kuielewa miiko, shabaha, maadili, nidhamu ya chama, sera na utamaduni wake

Pia, hutakuwa kwanza apigwe msasa kupitia madarasa ya itikadi, ajifunze na kujua mantiki na tafsiri ya siasa ya chama, malengo ya kuundwa kwa chama hicho ,kujua madhumuni yake, sera zake zikoje ndipo awive hatimaye aitwa kada wa CCM.

Kwa upande mwingine Chama Cha Mapinduzi kimewataka wanachama wake kuendeleza utamaduni wa kujitolea kwa ajili ya uhai na ustawi wa chama chao.

Makamu huyo Mwenyekiti akiweka mawe ya msingi katika uzinduzi au ujenzi wa ofisi za CCM wilaya kuanzia Misenyi mkoani Kagera hadi Sengerema mkoani Mwanza.

Kinana amesema, kazi za kujitolea kwa ajili ya maendeleo ya chama ni jambo linalitokana na historia ndani ya ccm kwani kazi hiyo imeanza tokea enzi kuvijenga vyama vya ukombozi vya TANU na ASP.

Amesema, hata aliyekuwa Rais wa TANU Marehemu Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere alipokwenda UNO mwaka 1958 kuielezea dunia Tanganyika iko tayari kujitawala nauli iliomfikisha huko ni michango ya wanachama wake.

Kinana amewahimiza wanachama wa CCM kuendelea na moyo wa kujitolea kwa ajili ya kustawisha mustakabali wa chama chao, kulinda heshima ya chama hicho, lakini pia akisema bila ya CCM yenye kutumikia watu nchi yetu itayumba.

Ametaka hadhi ya CCM lazima ifanane na majengo ya ofisi zake, iwe na viongozi bora ambao wamejitolea kutumikia Taifa kuanzia ngazi za matawi hadi Taifa.

Dhana ya usimamizi na uwajibikaji

Kinana amewakumbusha viongozi wa chama wakiwemo wabunge, wawakilishi na madiwani kuiwajibisha Serikali ya chama chao kwa nia ya kukijenga chama ndani umma kwani kazi hiyo ya kukosoa isipofanywa na wao hadi wananchi kufikia kuiwajibisha ni jambo la hatari.

Kukosoa kwa nia njema na kuielekeza Serikali na chama hakuna ubaya wowote. Serilali lazima ibanwe ili itoe majibu yatakayowaridhisha wananchi kutokana na chamgamoto mbalimbali zinazowakabili.

Serikali inapojibu, kufafanua, kuelezea na kuonyesha mambo kwa ushahidi, hoja kwa hoja au kwa swali na jibu sahihi; huo ndiyo uwajibikaji unaotakiwa kuonwa na wananchi dhidi ya Serikali iliyo madarakani.

Endapo Wawakilishi, Wabunge na madiwani kwenye halmashauri zao watasimama kidete usiku ma mchana kulinda fedha za umma, kufuta au kutotunga sheria kandamizi hapo ndipo watakapowapa nafuu wananchi dhidi ya maonevu na manyanyaso.

Uzinduzi wa miradi ya maendeleo

Baadhi ya watu inaoonekana hawajui nini msingi, maana na mantiki ya uzinduzi wa miradi ya maendeleo ya kisekta ikizinduliwa na viongozi wa CCM badala ya watendaji wa Serikali.

Kinachoonekana watu hao wenye fikra na mitazamo ya aina hiyo hawajui jinsi serikali inavyowekwa madarakani chini ya mfumo wa demokrasia ya chama kimoja au vyama vingi.

Washindi wa uchaguzi waliouza sera zao kwa wananchi wakati wa kampeni ndio wenye dhamana ya kufuatilia na kujua lipi na lipi lililoahidiwa na chama linatekelezwa kwa mujibu wa utekelezaji wa kisera na sio blabla.

Kazi ya ufuatiliaji miradi mi kazi maalum ya viongozi wa CCM ili kubaini mapema mambo yepi yamekwenda sawia, kwanini yakwame au iweje ishindakane hatimaye ufumbuzi upatikane.

Akiwa mkoani Kigoma akatembelea kuona maendeleo ya ujenzi wa bandari ya ujiji, lakini vile vile akashuhudia ukarabati wa meli mbili za MV Liemba na MT Sangara unavyoendelea ma kushauri masuala kadhaa ya msingi kwa shirika la badari .

Aidha, ameona maendeleo ya ujenzi wa barabara toka Kasulu hadi Nyakanazi na kuwahimiza wakandarasi wazidishe kasi ya ujenzi huo ili barabara hiyo muhimi iweze kuwasaidia wananchi kufanya shighuli za uzalishamali na kujijenga kiuchumi.

Ukiritimba, urasimu na ushirika

Akiwa wilayani Muleba mkoa wa Kagera, Kinana amevinyooshea kidole Vyama vya Ushirika. Hakuacha kuvizumgumzia vyama vya vya ushirika na vyama vya msingi akionyesha masikitiko yake,

Kinana akasema, lazima vyama hivyo viwe mkombozi kwa wakulima (wananchi) badala ya kuwa vyama vya kinyonyaji dhidi ya jasho la wakulima. Akaenda mbali na kusema iweje vyama hivyo viwe na viongozi ambao hata ekeri moja ya kilimo hawana

Alisema, ushirika usiowapa tija na manufaa wakulima huku baadhi ya viongozi wake wakiwa si wakulima hauwezi kuleta mageuzi na ukombozi wa kweli kwa wakulima ushirika huo unatia shaka.

Kinana akalizumgumzia zao la kahawa, huku akizitaka baadhi ya mamlaka kuacha kunyanyasa wakulima wa zao la kahawa ma wananachi wengine kwa kuwasumbua kwa kuweka tozo zenye kunyonya jasho lao.

Licha ya kuviasa vyama vya ushirika kuacha kuwapanga bei wakulima wanapotaka kuuza mazao yao pia amesisitiza ikiwa mkulima hakusaidiwa na vyama hivyo wakati wa kulima, kutafuta pembejeo, masoko na ushirika haiwezekani waamriwe kupangiwa bei ya kuuza kahawa yao.

Alisema, nguvu ya soko ndio inayopanga bei sokoni na wala isiwe shuruti kwa mkulima kupangiwa masharti wapi wauze mazao yao endapo wanajua mahali fulani watapata bei nzuri yenye faida kwao ili wajikwamue na umasikini

Aidha, Kinana amempa ushauri Mkuu wa Mkoa wa Kagera Albert Chalamila kuhakikisha anamaliza migogoro ya ardhi iliyopo mkoani mwake kwa njia za maelewano, mapatano na kwa mujibu wa sheria ili wananchi waishi kwa furaha.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here