Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimesema kuna dhana potofu kwa baadhi ya watu kudhani maendeleo yaliofikiwa Tanzania, yametokea kama miujiza na kusahau utashi wa viongozi, juhudi na uongozi bora.
CCM kimesisitiza maendeleo yalishamiri hivi sasa Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ujumla ni matokeo ya uongozi wenye hekima, busara na shime ya utekelezaji wa mipango na sera ya utekelezaki.
Tamko hilo limetolewa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itakadi, Uenezi Mafunzo, Komredi Khamis Mbeto Khamis, 28 Novemba 2026, ofisini kwake Kisiwandui, alipotembelewa na makundi ya viongozi wa Jumuiya ya Wazalendo Huru.
“Kuifikisha Tanzania mahali ilipo, haikuwa kazi nyepesi, hivyo mtu anapodhani maendeleo haya yametokea kimazingaombwe, hizo ni akili duni na fikra mgando,” alisema.
Alisema, Tanzania imejengwa chini ya misingi yake imara, iliowekwa toka awamu ya kwanza hadi hivi sasa ya sita, kwa kufanikiwa kupata viongozi wenye nia njema na dhamira thabiti ya kuliongoza Taifa.
Mbeto aliwaambia viongozi wa jumuiya hiyo kuwa maendeleo yaliochomoza Tanzania Bara na Zanzibar, ni uthibitisho wa juhudi kubwa chini ya uchapakazi wa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan na Dkt. Hussein Ali Mwinyi .
“Wanaodhani maendeleo duniani hutokea kimiujiza wanafanya makosa, hayachipui kama mchicha nyakati za mvua ya masika. Maendeleo ni mchakato unaobeba utashi wa viongozi, umakini, usimamizi wa sera na utekelezaji wa mipango kimkakati,” alisema.
Katibu huyo alibainisha kuwa Tanzania kutokana na kuwa na misingi madhubuti ya kihistoria na uongozi uliotukuka, ndio maana kila anayejaribu kutaka kuitoa katika reli yake halisi, hujikuta akikwama.
“Ni mwiko kufikiria maendeleo yanaweza kutokea baada ya mtu kulala na kuamka. Wanaobisha wakatembee mikoani na kujionea kazi iliofanyika kisha wailinganishe Tanzania ya sasa na nchi zingine Afrika,” alieleza.
Komredi Mbeto alisema, ni jambo la kujivunia kwa Tanzania kuiona inatekeleza miradi mikubwa ya kisekta toka ngazi za Vijiji hadi Mijini, ikiwemo ya elimu, usambazaji nishati ya umeme, huduma za afya, kilimo, maji Safi na salama, uvuvi na mifugo.
Aliwaeleza viongozi hao na kusema nchi nyingi duniani zimekuwa zikishangazwa na kasi ya maendeleo ilizofikiwa Tanzania Bara na Zanzibar.
“Wanaobeza Tanzania hakuna maendeleo hawajafika katika mikoa ya Tanzania Bara na Zanzibar . Tanzania ya leo si ile ya Mwaka 1961 kwa Tanzania Bara au Zanzibar ya Mwaka 1964,” alisisitiza.
Kadhalika Mbeto aliahidi kuwa chama na serikali zake zitaendelea kusimamia misingi ya amani, umoja na utulivu na kwamba mtu au kundi litakalovuruga amani iliopo, halitaachwa litambe.
“Tunaipa heko awamu ya sita kwa Tanzania na awamu ya nane Zanzibar kwa kazi kubwa yenye kuonekana.
Kila Mtanzania ana wajibu wa kujivunia matunda haya ya maendeleo yaliofikiwa nchini,” alisema Mwenezi huyo.