TIMU ya Elimu kwa Umma ya Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) imeendelea na kampeni ya kutoa elimu kwa wananchi, hususan vijana, kupitia ziara katika maeneo mbalimbali ya Wilaya za Kondoa, Chemba na Bahi, pamoja na Chuo cha Hombolo na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).
Ziara hiyo inalenga kuwajengea vijana uelewa kuhusu majukumu ya UCSAF, miradi inayotekelezwa katika kuhakikisha huduma za mawasiliano zinawafikia wananchi wote, pamoja na fursa zinazopatikana kupitia maendeleo ya teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA).
Aidha, vijana wanapata fursa ya kufahamu namna huduma za mawasiliano na teknolojia za kidijitali zinavyoweza kuwawezesha kupata maarifa, kukuza ubunifu, kuanzisha shughuli za kiuchumi na kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kidijitali.
Kupitia elimu hii, UCSAF inalenga kuhakikisha vijana si watumiaji wa huduma za mawasiliano pekee, bali pia wanakuwa wanufaika na washiriki muhimu katika kutumia teknolojia kuleta mabadiliko chanya katika jamii.