Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimempongeza Mwenyekiti wake Rais Dkt. Samia suluhu Hassan kwa kukata utepe na kutandika zulia la majadiliano yenye lengo la kufikia muafaka wa kitaifa nchini
Pia, chama hicho kimetaja nia njema ya Rais , chini ya Kanuni yake ya Nne, nia ni kuziba nyufa na kuliunganisha Taifa hatimae kufikia muafaka wa pamoja.
Pongezi hizo zimetolewa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis , aliyesema nia njema ya Rais Dkt. Samia, ndiyo dira sahihi yenye mwelekeo chanya.
Mbeto alisema, kwa Vyama vyote makini vya kisiasa vinavyothamini Umoja, Amami na Utulivu, havitakwepa kushiriki katika Meza ya mazumgumzo yanayokusudia kuondosha dosari, hitilafu na kasoro zozote.
Alisema, Chama Cha Mapinduzi kwa dhati kabisa, kinampongeza Mwenyekiti wake Rais Dkt. Samia, kwa juhudi kabambe zitakazohakiksha Taifa linasongambele kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.
“Kamwe hatutabweteka na kubeza mantiki ya mazungumzo yenye kufikia utatuzi. Vyama vyote vya kisiasa vina haki na wajibu wa kujitafakari. Hatuna wa kumngoja ajae kutuelekeza namna ya kufanya,” alisema Mbeto.
Katibu Mwenezi alisema kila chama kina ulazima wa kuhakikisha nchi yetu inabaki moja, na wala haitozama aidha katika mkondo wa Udini, Ukanda au Ukabila, hivyo kila mmoja ana wajibu wa kutambua umuhimu wa kushiriki mchakato wa upatanishi.
‘Tanzania ina sifa ya kuzikutanisha nchi mbalimbali katika meza moja ya majadiliano na kuzipatanisha pale zinapokuwa na hitilafu au migogoro. Hivyo, hatutashindwa kujadili jambo lolote linalotuhusu na kulipatia suluhu sisi wenyewe,” alisema Mbeto.
Aidha, Katibu huyo Mwenezi alisema mazumgumzo au majadiliano, ndio njia pekee inayoweza kuiweka pamoja jamii yoyote, pale zinapotokea dosari na kuzimaliza kwa njia za kiustarabu na kiungwana.
“Si uhodari kila chama kizungumza nje ya meza ya majadiliano. Huko ni kupoteza wakati . Mnapokutana meza moja kila upande hutaja hofu zao, wasiwasi walionao na kupendekeza njia bora za kufikia makubaliano imara,” alisisistiza.
Mbeto aliongeza kusema kuwa, msingi wa mazumgumzo yenye ajenda, miongozo na taratibu za kujadiliana kwenu, siku zote hutoa mwelekeo chanya wa kufikia mapatano thabit hatimae ukurusa mpya wa utekelezaji ukajiandika.
“Hakuna linaloshindikama mbele ya meza ya mazumgumzo. Tunapozungumzia leo kuwepo kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar ni matokeo na matunda ya mazungumzo yaliofungua ukurasa wa maridhiano hayo,” alisema Katibu Mwenezi huyo.