SERIKALI kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), imewekeza Shilingi bilioni 17.7 katika usambazaji wa vifaa vya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano-TEHAMA.
Mbali na vifaa hivyo, UCSAF inaendelea na ujenzi wa maabara za kompyuta katika shule za umma nchini, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kupunguza pengo la Kidijitali na kuboresha ufundishaji na ujifunzaji.
Akizungumza Jijini Dar es Salaam katika kikao kazi kati ya UCSAF, wahariri na waandishi wa habari kilichoratibiwa na kuandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina, Mkurugenzi wa Idara ya Uendeshaji, Utafiti na Maendeleo wa mfuko huo, Mhandisi Albert Richard, amesema uwekezaji huo umewezesha shule za umma 1,167 kunufaika hadi kufikia Oktoba 2026.
Mhandisi Richard, aliyemwakilisha Afisa Mtendaji Mkuu wa UCSAF, amesema mpango huo ni sehemu ya mkakati wa Serikali kuhakikisha wanafunzi wanapata fursa sawa za kujifunza na kutumia teknolojia, hususan katika maeneo ambayo yamekuwa na changamoto ya upatikanaji wa huduma za kidijitali.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina, Sabato Kosuri, amewataka wahariri na waandishi wa habari nchini kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu majukumu, uwekezaji na mchango wa taasisi na mashirika ya umma katika kukuza uchumi na kuboresha maisha ya wananchi.
Ameeleza kuwa ushirikiano kati ya taasisi za umma na vyombo vya habari ni muhimu katika kuhakikisha wananchi wanafahamu miradi inayotekelezwa na manufaa yake katika maendeleo ya taifa.