Na Mwandishi Wetu
CHAMA cha Mapinduzi (CCM) kimetaja ziara za Rais wa Zanzibar Dkt. Hussein Ali Mwinyi nje ya nchi moja ya malengo yake ni kupata suluhisho la kudumu la Umeme visiwani Zanzibar.
Pia, ziara zake zinakusudia kuongeza tija ya uzalishaji wa ndani na matumizi ya Nishati mbadala.
Matamshi hayo yametamkwa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis, kufuatia swali aliloulizwa kuhusu ziara za nje za Rais Dkt. Mwinyi.
Mbeto akijibu swali hilo alisema, tayari Rais akiwa Mjini Yeosu, Korea Kusini, amekutana na uongozi wa kampuni ya WongWang Electric Power Corporation (WG Corporation).
Katika kikao hicho pande mbili, zimezungumzia changamoto na fursa za Ushirikiano katika Uzalishaji, Uhifadhi na Usambazaji wa Umeme.
Aidha, chama hicho kimesisitiza kitazidi kuishauri Serikali ili iendelee kuyatumia majuukwaa mapya na yake yaliojengwa na viongozi wa Awamu zilizopita ili nchi ipige hatua za kimaendeleo.
Mbeto alisema, Kampuni hiyo ya Korea iko tayari kutuma Wataalamu wake kuja Zanzibar, kufanya tathmini ya mahitaji ya kiufundi kwa ajili ya kubaini maeneo ya uwezekano wa kutekeleza miradi ya Nishati.
“Katika ulimwengu unaokabiliwa na ushindani Rais wa nchi hajifungii Ikulu. Baadala yake hutoka na kushiriki katika mawindo ya kiuchumi. Kama si yeye mwenyewe Wasaidizi wake hubeba majukumu hayo,” alisema Mbeto.
Akiitaja hatua hiyo alisema, inalenga kuongeza uhakika wa upatikanaji Umeme, kupunguza Utegemezi wa Nishati hiyo kutoka Tanzania Bara na kuweka msingi madhubuti ya Maendeleo endelevu Zanzibar.
“Akimaliza ziara yake huko Yeosu, Rais Dkt. Mwinyi ataelekea Kisiwa cha Jeju kushiriki Jukwaa la 27 la Sera za Utalii kwa Visiwa (ITOP Forum 2026). Jukwaa hilo litajadili Utalii endelevu na kuimarisha Ushirikiano wa maendeleo baina ya Zanzibar na Korea,” alieleza.
Pia, Mwenezi huyo alisema tija ya kushiriki katika majukwaa ya Kimataifa, Kikanda na yanayowashrikisha wana taaluma ni masuala mtambuka katika ulimwemgu mpya.
“Kiongozi wa Nchi hasafiri kwa ajili ya kutalii bali kwa malengo mahusus ya kuipigania nchi na watu wake kimaendeleo.” alieleza.
Mbeto alisema, mabadiliko ya kimaendeleo yanayoendelea kuchomoza Unguja na Pemba, yanatokana na mikakati ya ushirikiano, ushiriki na ushirikishwaji katika dunia ya leo.
Mbeto alisema, Rais Dkt. Mwinyi atakuwa akisafiri mara kwa mara duniani, kwa lengo la kuingia kwenye mawindo ya Kiuchumi, kujifunza ili kujenga ushawishi mbele ya uso wa dunia.