Na Mwandishi Wetu
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimempongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa kutekeleza ahadi ya Serikali yake kupandisha Mishahara ya Wafanyakazi.
Pia, CCM kimeitaja hatua hiyo ni utekelezaji unaothibitisha azma ya SMZ ya kupandisha Mishahara kutokana na nia safi alionayo Rais huyo.
Pongezi hizo zimetolewa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis huko Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui Kisiwani Unguja.
Mbeto alisema, siku zote ahadi huwa zaidi ya deni na pale ahadi inapotekelezwa, huthibitisha uungwana wa mtu alieahidi na kutimiza ahadi yake .
Alisema, kitendo cha Serikali ya Awamu ya Nane kupandisha Mshahara kwa kima cha chini toka laki 3 hadi 5 kwa Mwezi, kinapaswa kuuungwa mkono na kupongezwa.
“Chama Cha Mapinduzi kwa dhati kabisa kinampongeza Rais Dkt. Mwinyi kwa hatua ya Serikali yake kupandisha kima Cha chini cha Mishahara. Pia nyongeza hiyo ya Mishahara imefanyika kwa Wafanyakazi wa madaraja mengine,” alisema Mbeto.
Katibu huyo Mwenezi alisema, Mei Mosi Mwaka huu katika Maadhimisho ya siku ya Wafanyakazi Duniani, Rais Dkt. Mwinyi aliahidi kuwa serikali yake itaongeza mishahara kwa wafanyakazi wa SMZ.
Sherehe za Mei Mosi zilifanyika huko Dole Kizimbani Wilaya ya Magharibi A, Mkoa wa Magharibi Kisiwani Unguja.
“Waswahili husema Ada ya mja hunena uungwana ni vitendo. Ahadi ya Rais Dkt. Mwinyi imetimia kwa Wafanyakazi wote wa Serikali. Yote yalioahidiwa yataendelea kutekelezwa ,”alisisitiza.
Aidha, Katibu huyo Mwenezi aliwataka Viongozi dhamana wa serikali katika upandishaji viwango vya Mishahara katika Wizara,Taasisi, Idara na kwenye Vitengo vya SMZ, kusitokee urasimu utakaoleta manung’uniko katika upandishaji Mishahara mipya.
“Kazi ya upandishaji mishahara kwa madaraja yote itaanza rasmi Mwezi huu. Itapendeza endapo hakutojitokeza malalamiko toka kwa Mfanyakazi wa daraja lolote,” alishauri Mbeto.