π Vikundi 42 vyapatiwa mikataba ya Milioni 473
π Wananchi wanufaika na matengenezo ya barabara
WAKALA ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mkoa wa Mara umefungua fursa za ajira na kuongeza ushiriki wa wananchi katika kulinda miundombinu ya barabara kupitia mpango wa Matengenezo ya Kawaida ya Barabara kwa Ushirikishwaji wa Jamii (CBRM), ambapo vikundi 42 vimesaini mikataba yenye thamani ya Shilingi Milioni 472.99.
Vikundi hivyo ambavyo vinatoka katika Halmashauri za Manispaa ya Musoma, Musoma Vijijini, Tarime Mji na Tarime Vijijini vimepewa mikataba pamoja na vifaa vya kufanyia kazi ili kutekeleza shughuli za matengenezo ya kawaida ya barabara, hatua inayolenga kuimarisha miundombinu ya barabara pamoja na uwezeshaji wa wananchi kiuchumi.
Meneja wa TARURA Mkoa wa Mara, Mhandisi George Tarimo amesema kupitia mpango huo vikundi vitashiriki katika kazi mbalimbali zikiwamo kusafisha na kuzibua mifereji na makalavati ili kuhakikisha maji yanapita vizuri, kufyeka nyasi na kuondoa vichaka kandokando ya barabara, kuziba mashimo madogo madogo na kuondoa vizuizi vinavyoweza kuhatarisha usalama wa watumiaji wa barabara.
βUshiriki huo unatarajiwa kuongeza fursa za ajira katika jamii, huku fedha zinazopatikana kupitia mikataba zikichochea shughuli za kiuchumi na kuongeza kipato cha wanavikundi na familia zaoβ.
Aidha, ameongeza kuwa mpango huo unalenga kuongeza uwajibikaji na umiliki wa wananchi katika utunzaji wa miundombinu, kwa kuwa watu wanaoishi karibu na barabara wanapata nafasi ya kushiriki moja kwa moja katika kuhakikisha zinakuwa salama na zinapitika mwaka mzima.
Katika mwaka wa fedha 2026/2027, TARURA Mkoa wa Mara unatarajia kutumia Shilingi Milioni 1,099 kwa ajili ununuzi wa vifaa vya kufanyia kazi kwa kila kikundi,usimamizi na matengenezo ya kazi za barabara kwa kutumia vikundi vya kijamii.