Na Aisha Swahibu, WAF
KWA mujibu wa Takwimu zilizotolewa katika kikao kazi cha tathmini ya mwaka ya huduma za afya ya uzazi Kanda ya Kaskazini, zinaonesha kuwa vifo vitokanavyo na uzazi vimeendelea kupungua kutoka vifo 168 mwaka 2021 hadi vifo 102 mwaka 2025 kati ya vizazi hai 100,000, huku msisitizo mkubwa ukitolewa juhudi zaidi kuendelea kufanyika ili kuendelea kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi endapo kila mmoja katika nafasi yake atatimiza wajibu.
Hayo yameelezwa jijini Tanga na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya kina mama kutoka KCMC ambaye pia ni Kaimu mwenyekiti wa kanda Dkt. Bariki Mchome wakati akifungua kikao kazi cha tathmini ya mwaka ya huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto kwa Kanda ya Kaskazini.
Amewataka wasimamizi wa huduma katika ngazi ya halmashauri na mikoa kuhakikisha uwepo wa kanzi data za kufuatilia mama na mtoto na kuchukua hatua kwa wakati.
Dkt. Mchome ameeleza kuwa kupungua kwa vifo hivyo kumetokana na jitihada kubwa zinazofanywa na watumishi wa afya wanaohudumia wananchi usiku na mchana, sambamba na kipaumbele cha Serikali katika kuboresha afya ya uzazi na watoto wachanga.
Amesema katika kutekeleza azma hiyo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kupitia Idara ya Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto, ameanzisha huduma za kambi za matibabu za Madaktari wa Mama Samia zinazozunguka nchini kwa lengo la kuwajengea uwezo kwa vitendo watoa huduma katika kukabiliana na dharura za mama na mtoto.
Aidha, Dkt. Mchome amewataka washiriki wa kikao hicho kujadili kwa kina sababu zinazochangia vifo vya akina mama vitokanavyo na uzazi na vifo vya watoto wachanga katika mikoa na halmashauri zao, ili kuandaa mikakati madhubuti ya kuhakikisha vifo hivyo vinaendelea kupungua na ikiwezekana kutokomea kabisa.
Amesisitiza pia umuhimu wa kuweka mikakati ya kuboresha huduma kabla ya kujifungua, wakati wa kujifungua na baada ya kujifungua, pamoja na kuboresha miundombinu na upatikanaji wa vifaa tiba katika vituo vinavyotoa huduma za mama na mtoto.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Wizara ya Afya kutoka Idara ya Afya Uzazi, Mama na Mtoto Bi. Jackline Ndanshau amesema lengo la kikao kazi hicho ni kuendelea kuweka mikakati ya kuendelea kupunguza vifo vya mama na mtoto, amewataka washiriki wa kikao hicho kuishi kwa vitendo kauli mbiu ya kikao isemayo “uongozi na uwajibikaji ni chachu katika kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi”
Dkt.Mchome pia ametoa pongezi kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uongozi na maono yake katika kuifanya afya ya mama na mtoto kuwa kipaumbele cha Taifa, akibainisha kuwa juhudi hizo zimetambulika kimataifa baada ya Rais kupokea mwaka 2022 tuzo ya Global Goalkeeper Award kwa mchango wake katika kuboresha huduma za afya, ikiwemo afya ya mama na mtoto.