Mkurugenzi wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) Masha Mshomba akizungumza katika mkutano wa Wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari ulioratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina.
Na Mwandishi Wetu
MFUKO wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umeendelea kupunguza muda wa kushughulikia madai ya wanachama ambapo hadi kufikia Juni 2026, asilimia 99 ya madai yote yaliyolipwa yalifanyiwa kazi ndani ya muda wa kisheria wa siku 60.
Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha Mshomba alisema hayo kwenye kikao kazi na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari, kilichoratibiwa na Ofisi ya Msajili Hazina na kuweka wazi kwamba, lengo la mfuko ni kwenda zaidi ya kiwango hicho kwa kutumia teknolojia.
Alisema, Ofisi ya Msajili wa Hazina imekuwa ikiihimiza NSSF kuongeza matumizi ya teknolojia, kuboresha ufanisi na kuondoa usumbufu unaoweza kusababishwa na ucheleweshaji wa malipo ya mafao.
Mbali na hayo, Mshomba alisema, NSSF imeendelea kuwezesha waajiri na wanachama kupata huduma mbalimbali bila kulazimika kufika katika ofisi za mfuko.
Alisema, matumizi ya mifumo ya Kidijitali yamekuwa sehemu muhimu ya mkakati wa kuboresha huduma, kuongeza ufanisi na kuimarisha usimamizi wa shughuli za mfuko.
Akifafanua zaidi Mshomba alisema, teknolojia pia ni sehemu ya dhana mpya ya NSSF ya kutoa huduma bora za hifadhi ya jamii kupitia watumishi wenye weledi na teknolojia inayokidhi mahitaji ya wakati.
Alisema, mfuko huo umefanya maboresho makubwa katika skimu yake ya hifadhi inayolenga watu waliojiajiri na wale wanaofanya shughuli katika sekta isiyo rasmi.
Alisema, mfumo wa awali ulikuwa na changamoto kwa sababu ulihitaji watu waliojiajiri kuchangia kwa utaratibu ambao haukuendana kikamilifu na mazingira ya kipato chao.
Mshomba alisema, tofauti na waajiriwa wenye mshahara wa kila mwezi, watu waliojiajiri wanaweza kupata kipato kinachobadilika kulingana na msimu, biashara au shughuli wanazofanya.
Kutokana na hali hiyo, NSSF imeweka utaratibu unaotoa nafuu katika uchangiaji ambapo mwanachama anaweza kuchangia kiwango cha chini cha Shilingi 30,000, huku akihimizwa kuchangia zaidi kwa kuwa kiwango cha mafao kinategemea pia kiwango cha michango.
Aidha, mwanachama anaweza kuchangia kwa siku, wiki, mwezi au miezi kadhaa, huku akiruhusiwa kulipa michango ya mapema kwa kipindi kinachoruhusiwa na utaratibu wa skimu.
Alisema, maboresho hayo yameanza kuonyesha matokeo, akieleza kuwa hadi Juni 2026, skimu hiyo ilikuwa na wanachama 577,791.
Alisema, NSSF inalenga kuongeza kwa kiasi kikubwa idadi hiyo katika kipindi cha mpango mpya wa maendeleo, hasa kwa kuwafikia waliojiajiri na wafanyabiashara katika sekta isiyo rasmi.
Pia, Mkurugenzi huyo alisema NSSF imeboresha baadhi ya mafao kwa wanachama wake, ikiwemo kuongeza kiwango cha chini cha pensheni ya kila mwezi.
Alisema, kiwango hicho kimeongezeka kutoka Shilingi 100,000 hadi Shilingi 150,000 ambapo maboresho hayo yanalenga kuongeza ulinzi wa kijamii kwa wastaafu, huku akieleza kuwa kiwango cha mafao kinahitaji kuangaliwa kwa kuzingatia uwezo wa uchumi na mazingira ya ajira nchini.
Katika hatua nyingine, Mshomba alisema, mwanachama anayefikisha umri wa miaka 60 bila kutimiza miezi 180 ya michango inayohitajika kwa ajili ya kupata pensheni ya kila mwezi amepewa fursa ya kuendelea kuchangia kwa hiari hadi kufikia umri wa miaka 70.
Alisema, utaratibu huo unalenga kumpa mwanachama nafasi ya kukamilisha sifa zinazohitajika na hatimaye kupata pensheni ya kudumu, ambapo lengo kuu la hifadhi ya jamii si kumlipa mwanachama fedha kwa mkupuo pekee, bali kuhakikisha anapata kipato endelevu baada ya kuacha kazi.
Mkurugenzi Mkuu huyo alisema, muda wa kusubiri malipo kwa baadhi ya wanachama wanaotoka kazini kabla ya kufikia umri wa kustaafu umefanyiwa maboresho.
Alisema, awali baadhi ya wanachama walilazimika kusubiri hadi miaka miwili katika mazingira yaliyokuwepo, lakini utaratibu mpya unaruhusu mwanachama anayekidhi vigezo husika kupata malipo ndani ya siku 90 baada ya kuacha kazi.
Aidha, amewataka wanachama kutanguliza uendelevu wa uanachama na pensheni ya baadaye pale mazingira yanaporuhusu, badala ya kukimbilia kuchukua mafao yote.
Mshomba alisema, bado kuna changamoto katika utekelezaji wa michango ya hifadhi ya jamii, ikiwemo baadhi ya waajiri kutotoa mikataba ya ajira na wengine kuwasilisha michango ambayo haiendani na idadi au mishahara ya wafanyakazi waliopo.
Alisema, NSSF imekuwa ikikabiliana na changamoto hizo kupitia elimu, ukaguzi na ushirikiano na taasisi za Serikali.
Mshomba alisema, mwajiriwa ana wajibu wa kufuatilia michango yake na kutoa taarifa endapo anabaini kiasi kinachowasilishwa kwa NSSF hakilingani na stahiki zake.