Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
MAKAMU Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo Zanzibar, Ismail Jussa Ladhu ametakiwa kuacha kutumia misamiati ya Utanganyika na Uzanzibari katika kile alichodai kuwa ni juhudi za kuwagawa na kuwagombanisha Watanzania.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis, ofisini kwake Kisiwandui, na kusisitiza kuwa Utanzania ni nguzo na msingi madhubuti uliojenga umoja, mshikamano na udugu wa damu kati ya Watanganyika na Wazanzibari ambao umeendelea kuwaunganisha kwa zaidi ya miaka 62 tangu Muungano wa mwaka 1964.
Alieleza kumshangaa Jussa kwa kile alichodai kuwa ni mwenendo wa kisiasa unaolenga kuibua tofauti kati ya wananchi wa Tanzania Bara na Zanzibar, akisema hatua hiyo ni juhudi hasi na aina ya ‘fitna za siasa za uke wenza’.
Akizungumza kuhusu kauli na mwenendo wa Jussa, Mbeto amesema anachokifanya ni kujaribu kujenga taswira kwamba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, anapendwa zaidi na Wazanzibari kuliko Watanzania wa Bara.
“Mwambieni Jussa aachane na aina ya siasa za uke wenza. Rais Dkt. Samia tangu aingie madarakani amekuwa kipenzi cha Watanzania wote. Aina ya uongozi wake haina tofauti na viongozi wenzake waliomtangulia,” amesema Mbeto.
Mbeto amesema, kwa wiki kadhaa Jussa amekuwa akijionesha kuwa na mapenzi makubwa kwa Zanzibar huku akiwakebehi wananchi wa Tanzania Bara, bila kuzingatia kuwa miongoni mwa wananchi hao wapo pia wanachama na wafuasi wa ACT-Wazalendo.
“Anachofikiria Jussa ni kujaribu kumgombanisha Rais Dkt. Samia na wananchi wake upande wa Tanzania Bara ili ionekane kama anapendwa sana Zanzibar. Dkt. Samia si Rais wa Wazanzibari pekee, bali ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” alifafanua.
Kuhusu historia ya uongozi wa Tanzania, Mbeto amesema viongozi waliowahi kuongoza nchi hawakuwahi kujifunga katika maeneo yao ya kuzaliwa, bali waliongoza Tanzania nzima.
“Julius Nyerere hakuwa Rais wa Butiama, Ali Hassan Mwinyi hakuiongoza Mangapwani wala Benjamin Mkapa hakuwa Rais wa Lupaso. Kadhalika, Jakaya Kikwete hakuitwa Rais wa Msoga, John Magufuli hakuitawala Chato na Dkt. Samia si Rais wa Kizimkazi,” alisisitiza.
Mbeto amemtaka Jussa kutambua hatua ambayo Watanzania wamefikia katika kujenga umoja wao, akisema hakuna mtu wala kundi lenye uwezo wa kuwagawa na kuwarudisha katika hali ya kabla ya Muungano wa mwaka 1964.
Amesema fikra za kuamini kuwa Tanzania inaweza kugawanyika kwa misingi ya maeneo au tofauti za kisiasa ni “ndoto za mchana na njozi za jinamizi”.
“Jussa acha fikra mgando kwa kudhani utafanikiwa kuwagawa Watanzania kwa utashi wako wa kisiasa. Waulize baba na kaka zako waliojaribu kufanya mtihani huo walifikia wapi,” alisema.
Mbeto amesisitiza kuwa, umoja wa Watanzania haupaswi kutumiwa kama nyenzo ya kutafuta maslahi ya kisiasa, akisema tofauti za kisiasa hazipaswi kugeuzwa kuwa chanzo cha kuwagawa wananchi kwa misingi ya Tanganyika na Zanzibar.
Ameongeza kuwa CCM, ACT-Wazalendo na vyama vingine vinaweza kuwa na tofauti za kisiasa, lakini hakuna sababu ya kutumia tofauti hizo kuwagonganisha viongozi au kuchochea migawanyiko miongoni mwa wananchi.
“Si Jussa, ACT-Wazalendo wala wenzake ambao wamewahi kuwa na upendo kwa CCM. Hivyo, majaribu yoyote ya kutaka kuwagonganisha viongozi au kuwafitini, ngoma hiyo itapasukia kwake,” alimaliza.