RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amekutana na Katibu Mkuu wa Makumbusho ya Taifa ya Oman, Jamal bin Hassan Al-Moosawi, kwa mazungumzo maalum yaliyolenga kuimarisha uhusiano na ushirikiano katika uhifadhi na uendelezaji wa maeneo ya urithi wa kihistoria na utamaduni wa Zanzibar.
Mazungumzo hayo yamefanyika Agosti 5, 2026, Ikulu Zanzibar, na kuhudhuriwa pia na Balozi Mdogo wa Oman Zanzibar, Balozi Said Salim Al-Sinawiy.
Rais Dkt. Mwinyi ameipongeza Serikali ya Oman kwa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika juhudi za kuhifadhi na kuendeleza urithi wake wa kihistoria na utamaduni kupitia mipango na miradi mbalimbali.
Amesema ushirikiano huo una umuhimu mkubwa katika kuhifadhi historia ya Zanzibar, kuendeleza utamaduni wake na kuongeza mchango wa maeneo ya urithi katika uchumi na maendeleo ya nchi.
Rais Dkt. Mwinyi ameihakikishia Oman ushirikiano wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kufanikisha programu na miradi inayotekelezwa Zanzibar, hususan katika uhifadhi, usimamizi na uendelezaji wa maeneo ya urithi wa kihistoria na utamaduni.
Aidha, ameiomba Oman kuendelea kushirikiana na Zanzibar katika kuimarisha programu za mafunzo na kujenga uwezo wa wataalamu wa ndani, hususan katika matumizi ya mbinu na teknolojia za kisasa za uhifadhi wa maeneo ya kihistoria, usimamizi wa urithi na utunzaji wa kumbukumbu.
Amesema hatua hiyo itasaidia kuongeza ufanisi na kuweka mifumo bora ya kuhifadhi urithi wa Zanzibar kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Makumbusho ya Taifa ya Oman, Mhe. Jamal bin Hassan Al-Moosawi, ameihakikishia Zanzibar kuwa Oman itaendelea kushirikiana nayo katika kuhifadhi na kuendeleza urithi wa kihistoria na utamaduni, pamoja na kumbukumbu muhimu za kihistoria, kiutamaduni na kijamii.
Amesema ushirikiano huo ni sehemu ya kuendeleza uhusiano wa muda mrefu uliopo baina ya Zanzibar na Oman na kuimarisha zaidi ushirikiano katika maeneo yenye maslahi ya pamoja.