Na Mwandishi Wetu
SHINIKIZO la kumtaka Makamu Mwenyekiti Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) John Heche ajiuzulu kutokana na tuhuma zinazomkabili za matumizi mabaya ya fedha za michango ya chama hicho, limeendelea kwenye maeneo mbalimbali nchini.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, viongozi na wanachama wa CHADEMA wamesema, wanataka kufanyike uchunguzi huru ili kubaini ukweli wa tuhuma hizo, huku wakisisitiza kuwa, lengo la msimamo wao huo ni kulinda maslahi ya chama na si kukidhoofisha.
Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Chadema (BAVICHA) Jimbo la Lushoto, Mkoa wa Tanga, Mambo Nassoro Mkuya, alisema wanachama wa kawaida ndio wanaobeba mzigo wa kukijenga chama na hivyo wanastahili kupata majibu kuhusu tuhuma zinazoibuliwa za matumizi mabaya ya fedha za chama hicho.
“Vijana ndio nguvu ya chama. Tunamuomba Makamu Mwenyekiti apishe uchunguzi ufanyike, kisha akibainika hana kosa atarejea kuendelea na majukumu yake. Tunataka ukweli ujulikane kwa sababu sisi ni watu wa hali ya chini tunaotoa michango kwa ajili ya chama,” alisema.
Katibu wa CHADEMA Wilaya ya Lushoto na Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake la Chadema (BAWACHA) wilayani humo, Jelda Ramadhani Ghosha alisema, wanachama wanahitaji majibu ya wazi kuhusu madai yanayoendelea kusikika.
“Kama madai hayo si ya kweli, uchunguzi utaonyesha. Kama ni ya kweli, hatua zichukuliwe. Tunataka ukweli ujulikane. Ninatambua kauli yangu inaweza kuniletea hatua za kinidhamu, lakini kabla ya hilo ningependa niitwe mbele ya vikao vya maadili nisikilizwe,” alisema.
Naye, Katibu wa CHADEMA Handeni Mjini na Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa wa chama hicho, Kombo Mohammed Maturu, alisema sintofahamu inayoendelea ndani ya chama imezua taharuki miongoni mwa wanachama.
Alisema, viongozi wa ngazi za chini wamekuwa wakikosa majibu kuhusu tuhuma zinazoelekezwa kwa baadhi ya viongozi wa juu wa chama hicho.
“Makamu Mwenyekiti ni mmoja wa viongozi tunaowategemea. Tunajiuliza kwa nini asipishe uchunguzi ili ukweli ubainike. Wanachama wanahitaji majibu badala ya kushambuliwa wanapouliza maswali,” alisema.
Maturu alimwomba Katibu Mkuu wa CHADEMA John Mnyika kuunda tume huru ya kuchunguza madai hayo ili kuondoa sintofahamu na kurejesha utulivu ndani ya chama.
Katibu wa BAVICHA Mkoa wa Pwani, Issa Ramadhani Mwaja alisema, ni muhimu kufanyika kwa uchunguzi wa madai yanayomkabili Heche ili kulinda maslahi ya chama na kurejesha imani ya wanachama.
Mwaja alisema, vijana wa CHADEMA hawawezi kunyamazia mwenendo unaodaiwa kukihatarisha chama kutokana na maslahi binafsi ya baadhi ya viongozi, akisisitiza kuwa viongozi wa sasa wanapaswa kuonyesha ujasiri wa kufanya maamuzi yatakayolinda mustakabali wa chama.
Aliongeza kuwa, bado kuna maswali kutoka kwa viongozi wa ngazi za chini kuhusu fedha zilizodaiwa kuahidiwa kupelekwa kwenye majimbo kwa ajili ya shughuli za chama, akidai kuwa fedha hizo hazijawahi kufika kama ilivyoelezwa.
Mmoja wa wanachama wa Chadema Gervas Mwambi alisema, wiki iliyopita amemsikiliza Makamu Mwenyekiti John Heche akiwa nyumbani kwao Tarime ambapo alitarajia angejibu tuhuma zinazomkabili au angetangaza kujiuzulu, lakini ameshangazwa na kauli za vitisho na ubabe alizozitoa.
“Nilitarajia baada ya ukimya wake wa muda mrefu tangu zilipoibuliwa tuhuma dhidi yake angetoa majibu yanayoeleweka au angejiuzulu, lakini badala yake ametoa vitisho na kauli za ubabe…Sisi sio mbwa, Makamu Mwenyekiti Taifa aache kauli za kibabe, awajibike,” alisema Mwambi.
Mbali na wanachama na viongozi hao wa Chadema, suala hilo limeendelea kujadiliwa na watu mbalimbali wakiwemo wachambuzi wa masuala ya kisiasa na viongozi wa vyama vingine vya upinzani akiwemo Kaimu Katibu Mkuu wa CHAUMA, Benson Kigaila.
Kigaila akizungumza na waandishi wa habari hivi karibuni jijini Dar es Salaam alisema, viongozi wanaowataka wengine wachunguzwe wanapaswa pia kuwa tayari kukubali uchunguzi wanapotolewa tuhuma zinazowahusu.
Alisema, ameshangazwa na msimamo wa baadhi ya viongozi wa CHADEMA, akiwemo Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, John Heche, kupinga uchunguzi kufuatia madai yaliyoibuka kuhusu matumizi ya fedha za michango ya wadau wa chama.
“Mnawaambia watu waendelee kuchangia fedha za chama, halafu zinapotokea tuhuma kuhusu matumizi ya fedha hizo, mnakataa hata zichunguzwe. Kama ni tuhuma, mbona msikubali zichunguzwe ili ukweli ujulikane?” alisema Kigaila.
Alisema, viongozi wanaotarajia kupewa dhamana ya kuongoza nchi wanapaswa kuonyesha mfano wa uwazi na uwajibikaji kwa kuwa tayari kujibu hoja na kuruhusu taratibu za uchunguzi pale panapozuka maswali kuhusu matumizi ya fedha au rasilimali wanazosimamia.
Kwa mujibu wa Kigaila, Tanzania inahitaji viongozi wanaojenga utamaduni wa uwazi, wanaokubali kuwajibika na wasiokwepa uchunguzi wanapotuhumiwa, ili kuongeza imani ya wananchi kwa taasisi na viongozi wao.
Aidha, wachambuzi wa masuala ya kisiasa wamesema, suala hilo iwapo halitachukuliwa hatua za haraka na vikao vya maamuzi vya chama hicho, CHADEMA itakuwa kwenye wakati mgumu na itapoteza mvuto kwenye siasa za Tanzania.
Walisema, licha ya kuwepo kwa mjadala mkubwa miongoni mwa wanachama wa chama hicho na wananchi, lakini chama hicho hakijachukua hatua za haraka za kuhakikisha uchunguzi wa wazi na huru unafanyika, jambo ambalo limezua hisia kwamba, huenda kinamlinda kiongozi huyo.
Waliongeza kuwa, iwapo chama hicho cha upinzani kinapigania uwazi, uwajibikaji na mapambano dhidi ya ufisadi katika ngazi ya Taifa, kilipaswa viwango hivyo hivyo vikatumika ndani ya chama chenyewe.
Wamesema, endapo Chadema itafanya uchunguzi wa wazi na kutoa taarifa kwa umma kuhusu matokeo yake, itaonyesha kuwa chama hicho kinaweka mbele maslahi ya taasisi kuliko ya mtu mmoja.
“Kama tuhuma zitaachwa bila majibu ya kuridhisha, zitaendelea kuathiri taswira ya chama na kuibua maswali kuhusu dhamira yake katika kupambana na ufisadi. Suala hili si la John Heche pekee, bali ni mtihani kwa CHADEMA kuhusu namna kinavyotekeleza misingi ya uwajibikaji kinayoihubiri kwa Serikali na viongozi wengine,”