Makamu Mwenyekiti wa Chadema John Heche
. Wanachama, viongozi wamtaka ajitathimini na kukuchukua hatua
. Waviomba Vyombo vya Dola, Msajili wa Vyama kuingilia kati
. Mwenyewe aibukia Tarime, akwepa kujibu tuhuma zinazomkabili
. Rwakatare: kufukuzana, kusimamishana uanachama hakusaidii lolote
Na Mwandishi Wetu
HALI ya kisiasa ndani ya chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)inaendelea kuwa mbaya, kufuatia tuhuma za matumizi mabaya ya fedha za michango zinazomkabili Makamu Mwenyekiti wa chama hicho John Heche.
Heche, anadaiwa kuhusika kwenye kashfa ya matumizi mabaya ya fedha za michango inayotolewa na wanachama na wadau wa chama hicho kupitia njia mbalimbali ikiwemo kampeni ya ‘Tone Tone,’ ambayo ilizinduliwa Februari, 2025.
Tuhuma hizo zilibuliwa na viongozi wa chama hicho kutoka mikoa mbalimbali, ambapo walikitaka chama hicho na Mamlaka mbalimbali kufanya uchunguzi wa madai hayo.
Viongozi hao walisema, chama chao kwa miaka mingi kimekuwa kikikemea matumizi mabaya ya fedha za umma na wamekuwa vinara wa kukosoa taasisi zinazotajwa kwenye Ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Fedha za Umma (CAG), hivyo hakikupaswa kuingia kwenye kashfa yoyote ya matumizi mabaya ya fedha.
Walisema, jambo baya zaidi ambalo linaendelea kukijengea chama hicho taswira mbaya, ni kitendo cha viongozi wa ngazi za juu kulindana na kukingia kifua tuhuma hizo, wakati kilipaswa kuwa mfano bora wa viongozi kujithathimini na kuchukua hatua kwa lengo la kuendelea kukijengea imani kwenye jamii.
Katibu Mwenezi wa Chadema Jimbo la Newala Mjini, Mkoani Lindi Ismail Chipalu, akizungumza na waandishi wa habari Julai, 15, 2026 amesisitiza uwajibikaji na kuomba Mamlaka husika kuingilia kati sakata hilo.
Chipalu amemuomba Msajili wa vyama vya siasa, Kamati Kuu ya Chadema na Bodi ya wadhamini wa chama hicho kuingilia kati, kwani chama hicho ni mali ya umma na fedha zake zinapaswa kutumika kwa uwazi.
Alisema, kuna fedha za wafadhili kutoka Ujerumani na zile zinazochangwa kupitia kampeni mbalimbali, zimekuwa zikiishia Makao Makuu ya chama hicho, badala ya kusambazwa kwenye mikoa mingine kwa ajili ya kusaidia shughuli za uendeshaji wa chama hicho.
Chipalu alisema, kutokana na ukosefu wa fedha, wamekuwa wakifanya kazi kwenye mazingira magumu, ambapo wanapoletewa maagizo ya utekelezaji wa ujenzi wa chama kutoka Makao Makuu, wanashindwa kuyafikisha kwa viongozi wa ngazi mbalimbali ndani ya Jimbo hilo.
“Siasa zetu zimekuwa ngumu kutokana na mazingira ya Kiutendaji, Jimbo letu lina kata tisa, lina vijiji 48, tunapata wakati mgumu kufanya siasa kwenye vijiji na kata zote kutokana na ukosefu wa vitendea kazi,” alisema na kuongeza kuwa, mwaka 2000 waliwahi kupewa pikipiki wakati wa uongozi wa Mwenyekiti Freeman Mbowe, lakini zimeharibika na hazifanyi kazi kabisa.
Alisema, kwa muda mrefu, yeye na wanachama wenzake, wamekuwa wakitumia fedha zao za mifukoni wanazozipata kutokana na shughuli mbalimbali wanazozifanya kukodi magari na kuweka mafuta kwa ajili ya kwenda vijijini kujenga chama.
“Kwa utaratibu huo tumefanikiwa kujenga chama kwa kiasi kikubwa kusimamisha viongozi kwenye kila kata, hata kwenye uchaguzi wa mwaka 2000 tulipata madiwani kwenye kata zote, waligombea kwa jitihada zetu bila msaada wa Chadema Makao Makuu,” alisema.
Aliendelea kusema, wakati wao wakihangaika na kupambana kukijenga chama katika mazingira magumu, wamesikitishwa na malalamiko yanayotolewa dhidi ya viongozi wa chama chao kuhusiana na matumizi mabaya ya michango ya wanachama na wafadhili.
“Tunaamini fedha zinatumika kinyume na utaratibu, anapotokea mwanachama akapaza sauti kuhusiana na matumizi mabaya ya fedha, suluhisho limekuwa kumfukuza uanachama na sio kujibu hoja kama mwanachama alivyoipeleka au kutafuta ufumbuzi, kwa mfumo huu tunajiuliza tutafukuza wanachama wangapi? Na hatma yake ni nini?” alihoji Chipalu.
Alisema, kwasasa hawajui kiasi cha fedha kinachoingia kwenye chama hicho, wala kinavyotumika wakati kila kitu kilipaswa kujulikana huku akishangazwa na barua za kufukuzwa uanachama na vitisho wanavyotolewa wanaohoji matumizi ya fedha hizo.
“Mwelekeo huu unaenda kukiangusha chama chetu, kwasababu viongozi tulionao sasahivi walipatikana kupitia uchaguzi wa wazi na kura zilikuwa za wazi na zikahesabiwa wakashinda, tulitarajia watuletee matunda, lakini matunda tuliyotarajia hatuyaoni,” alisema.
Aliendelea kusema “tonetone zinakusanywa sana na watu wanajitoa kwasababu chama kimeingia kwenye imani za watu kwamba ndio kitakuwa mkombozi wa Taifa hili na wanaochangia wana uchumi mdogo, ila kwa mapenzi yao ya moyoni wanajitoa,”
“Hawatoi kwa ajili ya kulea familia ya mtu au kumnunulia mtu mavazi, hawatoi kwa ajili ya kumpaulia mtu nyumba yake, wanatoa ili viongozi waendelee kushirikiana na viongozi wa chini kukijenga chama, lakini hayo ni mambo ambayo hayapo, hatuyaoni, kwa hiyo wale walioingia kutoa tuhuma kwa Makamu Mwenyekiti wa chama kwamba anakula fedha za chama, ninaungana nao, nawasapoti,” alisema Chipalu.
Kutokana na tuhuma hizo, Katibu Mwenezi huyo amemtaka John Heche kujitathimini na kuchukua hatua, kwani amekwenda kinyume na matarajio ya wanachama wengi ambao walitamani kuona mabadiliko makubwa kwenye chama hicho kwa kipindi chake cha uongozi.
“Sisi tunafanya kazi ngumu ya kukusanya wanachama kwenye chama chetu, halafu kuna watu wanajipatia pesa kwa njia nyepesi, hatukatai anafanya kazi nzuri ya kuzunguka kutoa elimu mikoani, lakini utaratibu unaotumika kwenye fedha kwanini uguse watu wachache wakati chama kina watu wengi?” alihoji.
Kwa upande wake aliyewahi kuwa kiongozi wa Kambi rasmi ya upinzani bungeni kwa tiketi ya Chama cha Wananchi (CUF), Wilfred Rwakatare, akizungumzia hatua ya Chadema kuwasimamisha viongozi wake waliohoji matumizi ya fedha, alisema hakuona sababu ya kuwasimamisha kwani badala yake walipaswa kuwaita na kuzungumza nao kisha kutafuta mwafaka.
“Kama chama ni cha demokrasia basi lazima kionyeshe mfano, huwezi kusema unaenda kuridhiana na Serikali wakati ndani mwako kunawaka moto, yaani umeshindwa kuridhiana na watu wako wa ndani, unawafukuza halafu unaenda kuridhiana kwingine badala ya kuanza na kwako, toa boriti ndani ya jicho lako kabla ya kutoa boriti kwenye jicho la mwingine,”
“Mimi naamini katika demokrasia ya kuzungumza, haiwezekani wote ndani ya chama mkawa mnakubaliana kwa kila jambo, kwa hiyo mkitofautiana mawazo lazima muweke utaratibu wa kwenda pamoja kwa kusikilizana badala ya kufukuza kila anayetoa maoni yake, mimi naona kufukuzana wala kusimamishana hakusaidiii lolote,”
“Wito wangu ni kwamba, demokrasia lazima ianzie kwenye vyama vyetu wenyewe yaani tumalize matatizo yetu kwa kuzungumza na wenye maoni tofauti na sisi maana haipendezi mnapambana wenyewe kwa wenyewe ndani halafu mnaenda kuridhiana wakati nyumba yenu inawaka moto,” alisema Rwakatare.
Hata hivyo, katika kile kinachotafisiriwa kwamba ni majibu ya kuhusu tuhuma zinazotolewa dhidi yake, Makamu Mwenyekiti wa Chadema John Heche, bila kujibu wala kuweka wazi kuhusu tuhuma zinazotolewa dhidi yake, amesema msimamo wake hauwezi kubadilika wala kutetereka.
Heche ameyasema hayo Julai 15, 2026, nyumbani kwake Tarime, mkoani Mara “mnayoita mashambulizi dhidi yangu wala sisikilizi, hayanipi shida waliokuwa wanajidanganya nitarudi nyuma, mimi ni mtu wa kutishwa mimi, yani kwamba unaweza kunirudisha nyuma kwa maneno ya mtaani hayo ya khanga khanga nikasikiliza Mimi nasonga mbele.”