Na Norah Msemwa
NILITAZAMA waraka wa ‘BBC Africa Eye’ kuhusu Tundu Lissu nikiwa na hisia zilizochanganyika.
Kama Mtanzania, niliguswa kuona mtu aliyenusurika jaribio la kutisha la kuuawa, akaishi uhamishoni, na sasa ametumia zaidi ya mwaka mmoja mahabusu akisubiri kusikilizwa kwa kesi ya uhaini inayomkabili.
Hakuna anayepaswa kubeza mateso ya kibinadamu yaliyoonyeshwa kwenye waraka huo, na kila Mtanzania anapaswa kutaka haki ipatikane kuhusu shambulio la mwaka 2017 ambalo bado halijapatiwa majibu, pamoja na kuhakikisha kuwa kesi ya sasa inaendeshwa kwa uwazi.
Lakini, waraka ulipoisha, nilijikuta nikiuliza swali tofauti: Ni nini kimeachwa nje? Na kwa nini kimeachwa nje? Uandishi wa habari hauhusu tu kile kinachojumuishwa; pia unahusu kile kinachoachwa.
Kwa mtazamo wangu,’ BBC Africa Eye’ imeandaa filamu yenye nguvu ya kihisia, lakini haijatoa taswira kamili ya mmoja wa wanasiasa wenye utata mkubwa nchini Tanzania.
Waraka huo unatuonyesha mateso aliyopitia Tundu Lissu, lakini hauzungumzi kwa kina namna alivyoendesha siasa zake na maamuzi yaliyomfikisha katika migogoro hiyo ya mara kwa mara.
Katika maisha yake ya kisiasa, Lissu amejijengea sifa ya kuwa mmoja wa viongozi wa upinzani wasiopenda maridhiano. Wafuasi wake humwona kama jasiri asiyeogopa.
Wakosoaji wake humwona kama mwanasiasa anayependelea migongano ya kisiasa. Vyovyote mtu anavyoweza kumwelezea, wengi wanakubaliana kwamba mara nyingi amechagua siasa za makabiliano badala ya maridhiano.
Hata ndani ya waraka huo, mke wake mwenyewe anaeleza athari ambazo familia imezipata kutokana na maisha yaliyojaa kesi mahakamani na vipindi vya kuwekwa mahabusu.
Hilo limewasilishwa zaidi kama ushahidi wa mateso aliyopitia. Lakini, linaweza kuwafanya watazamaji waulize, kwa nini mwanasiasa huyu amejikuta mara kwa mara katika migogoro ya kisheria kwa miongo kadhaa, ilhali viongozi wengine wa upinzani hawajapitia hali kama hiyo? Swali hilo linastahili kujadiliwa. Badala yake, waraka unaonekana kutoa jibu kabla hata ya kuuliza swali.
Moja ya mambo makubwa yaliyoachwa ni muktadha mpana wa uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan. Waraka unaonyesha kwa sekunde chache picha ya aliyekuwa Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan akimtembelea Lissu hospitalini mwaka 2017 alipokuwa akipata matibabu baada ya kushambuliwa.
Ilikuwa ni ishara ya ubinadamu licha ya tofauti za kisiasa. Hata hivyo, waraka hauchambui kwa kina maana ya tukio hilo wala mazingira ya kisiasa yaliyojitokeza baadaye chini ya uongozi wake.
Watanzania wanakumbuka kuwa muda mfupi baada ya kuingia madarakani, katika safari yake ya kwanza Brussels, Rais Samia alikutana hadharani na Lissu, akamkaribisha kurejea nchini na kuendelea na shughuli za kisiasa. Tangu wakati huo, serikali ililegeza baadhi ya vikwazo vya kisiasa na kuwezesha kurejea kwake kutoka uhamishoni.
Mambo hayo hayathibitishi kuwa kesi ya sasa ya uhaini haina masuala ya kisiasa. Lakini pia hayaungi mkono simulizi kwamba mateso hayo yalikuwa endelevu bila mabadiliko yoyote. Ukweli unaonekana kuwa mgumu zaidi kuliko simulizi rahisi.
Waraka pia unapita haraka katika sura muhimu ya hivi karibuni. Baada ya kurejea nchini, Lissu alikijenga upya CHADEMA, akafanya mikutano nchi nzima, akagombea na kushinda uenyekiti wa chama Januari 2025 kwa kumshinda Freeman Mbowe.
Kabla ya uchaguzi huo, katika mahojiano na BBC kwa Kiswahili na Sammy Awami, alisema wazi kuwa “hakuna tena kuimbiana mambo ya maridhiano yasiyokuwepo.” Alisisitiza kuwa uongozi wake ungejikita katika mapambano makali na kudai mabadiliko.
Waraka haujatoa uzito wa kutosha kuhusu kampeni ya “No Reforms, No Election”, uamuzi wa CHADEMA kutosaini kanuni za maadili ya uchaguzi, hatua iliyofuatiwa na kutoshiriki uchaguzi, pamoja na hoja ambazo waendesha mashtaka wanazitaja katika kesi ya uhaini.
Kilichonishangaza zaidi ni namna suala la maridhiano ya kisiasa lilivyoshughulikiwa. Mtindo wa Lissu umeonekana mara nyingi kupendelea makabiliano kuliko maelewano, si tu na serikali bali hata ndani ya chama chake.
Mwanasiasa anayepinga maridhiano ya ndani kabla ya kuchukua uongozi wa chama anaibua swali muhimu: Je, makabiliano yasiyo na nafasi ya maelewano ndiyo njia bora ya kuimarisha demokrasia? Watu wanaweza kutofautiana katika majibu yao, lakini BBC haikuliuliza swali hilo kwa kina.
Mimi si mtetezi asiyeona mapungufu ya hali ilivyo. Kama Watanzania wengi, ninaona changamoto katika utendaji wa serikali, kasi ya baadhi ya mageuzi na matatizo yanayoathiri maisha ya kila siku. Hata hivyo, Tanzania ndiyo nchi yangu.
Kutazama kutoka nje ya nchi kunanifanya nihisi maumivu makubwa kuhusu mwelekeo wa taifa letu, hasa baada ya migawanyiko iliyofuatia uchaguzi wa mwaka 2025.
Ninafurahia maendeleo ya uchumi, ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), bandari, miradi ya nishati, kuimarika kwa ushirikiano wa Afrika Mashariki na maono ya Dira 2050.
Wakati huohuo, naamini tunapaswa kuendelea kuimarisha taasisi, kulinda haki za kiraia na kuhakikisha haki inatendeka kwa uwazi huku tukidumisha utulivu unaovutia uwekezaji.
Hili linanileta kwenye swali muhimu, Wanawake wa Tanzania wako wapi? Wako wapi akina mama wanaoheshimika, wasomi, wafanyabiashara, majaji, viongozi wa dini, waandishi, wataalamu na viongozi wa jamii?
Kwa nini sauti za wanawake wachache sana zinasikika zikihimiza siasa za utulivu, mazungumzo ya kikatiba na uongozi wenye kuwajibika kutoka pande zote? Taifa limekaa kimya kwa kiwango kikubwa mno. Tunaweza kufanya vizuri zaidi.
Nikihusianisha swali hilo na waraka wa BBC, tofauti na lengo lililoonekana la watayarishaji wake, shujaa wangu ni Alicia Lissu. Simulizi yake ya utulivu ilizungumza zaidi kuliko picha zilizoonyeshwa.
Kama mwanamke, nilielewa zaidi hali anayopitia yeye kuliko simulizi la kisiasa la Tundu Lissu. Kumwona akiwa kando ya kitanda cha mume wake huku akishuhudia akifarijiwa na aliyekuwa Makamu wa Rais ilikuwa ni ishara ya matumaini kwake. Anawakilisha wanawake wengi wa Kitanzania waliochoshwa na migogoro ya kisiasa isiyoisha na wanaotamani ukurasa huu ufungwe.
Wakati huu ni mkubwa kuliko mwanasiasa mmoja, waraka mmoja au serikali moja. Tanzania inahitaji viongozi wa upinzani wanaoweza kuikosoa serikali kwa uwajibikaji. Inahitaji serikali zinazojibu ukosoaji kupitia taasisi badala ya kujihami.
Pia, inahitaji uandishi wa habari wa Kimataifa unaoeleza jamii kwa ukamilifu badala ya kuzigawanya katika simulizi rahisi za mashujaa na waovu. ‘BBC Africa Eye’ imefanikiwa kuwafanya watazamaji wamhurumie Tundu Lissu. Lakini haikufanikiwa kwa kiwango kilekile kuwasaidia kuielewa Tanzania.
Maswali kuhusu jaribio la kumuua Lissu mwaka 2017 yanahitaji majibu. Kesi ya sasa ya uhaini inahitaji kusikilizwa kwa haraka na kwa uwazi. Lakini, umma pia unastahili kupata picha kamili ya mtu aliyeko katikati ya simulizi hili—si mateso yake pekee, bali pia siasa zake, mbinu zake na maamuzi yake.
Ni hapo tu ndipo watazamaji wataweza kuamua wenyewe kama wanamtazama mwanamageuzi wa kidemokrasia, mwanasiasa anayependelea makabiliano, au kiongozi mwenye sifa za pande zote mbili. Hiyo ndiyo simulizi ambayo nilitarajia ‘BBC Africa Eye’ ingeisimulia.