RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Serikali inaendelea kutekeleza miradi mikubwa ya maji ili kumaliza tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama katika mikoa yote ya Zanzibar.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, Julai 15, 2026, Ikulu Zanzibar, alipokutana na Waziri wa Maji, Nishati na Madini Zanzibar, Nadir Abdullatif, pamoja na Waziri wa Maji wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jumaa Aweso.
Amesema miradi ya maji tayari imeanza kuleta matokeo katika mikoa ya Kaskazini Unguja, Kusini Unguja na Mjini Magharibi, huku akisisitiza matumizi ya teknolojia za kisasa na kuimarisha ushirikiano kati ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za maji.
Kwa upande wake, Waziri wa Maji wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jumaa Aweso, ameahidi kuendelea kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika utekelezaji wa miradi ya maji na kueleza kuwa wizara yake imeandaa mfumo wa Kidijitali utakaowezesha wananchi kutoa taarifa za changamoto za huduma ya maji ili zipatiwe ufumbuzi kwa haraka.
Vilevile, amempongeza Rais Dkt. Mwinyi kwa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayosimamiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.