Na Zakayo Mosha – WAF
SERIKALI ya Tanzania kupitia Wizara ya Afya inaendelea kuimarisha ushirikiano na Serikali ya Japan ili kuboresha huduma za dharura pamoja na kuendeleza elimu ya usalama barabarani kwa wananchi.
Elimu hiyo itatolewa kuanzia ngazi ya awali hadi elimu ya juu, ikiwa ni mkakati wa kupunguza vifo na madhara yatokanayo na ajali za barabarani nchini.
Hayo yamesemwa jijini Dodoma na Kaimu Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Eliud Eliakimu, wakati wa kikao cha wataalamu wa Wizara ya Afya, Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Japan (JICA) pamoja na Wizara ya Ujenzi.
Akizungumza katika kikao hicho, Meneja wa Mradi, Manabu Ohno amesema mradi huo umeanza Aprili 2025 na unatarajiwa kutekelezwa kwa kipindi cha miaka mitatu hadi mwaka 2028 na kuelezea kuwa mradi unalenga kutoa elimu kuhusu matumizi salama ya barabara kwa wananchi, hususan wanafunzi kuanzia shule za awali na msingi.
Dkt. Eliakimu amesema mafanikio ya mradi huo yanategemea ushirikiano wa karibu kati ya wizara na taasisi mbalimbali ili kuhakikisha unawafikia Watanzania wengi zaidi na kuchangia kufikiwa kwa malengo ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kupunguza vifo na madhara yatokanayo na ajali za barabarani ifikapo mwaka 2030.
“Ili mradi huu uendelee kufanikiwa na kuwafikia Watanzania wengi zaidi, juhudi na ushirikiano wa pamoja kati ya wizara za kisekta unahitajika ili kuhakikisha malengo ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kupunguza vifo na madhara yatokanayo na ajali za barabarani yanafikiwa ifikapo mwaka 2030,” alisema Dkt. Eliakimu.
Aidha, amewataka wataalamu kuendelea kukamilisha mikakati ya kitaalamu kwa kushirikiana na wizara na taasisi zinazohusika na huduma za dharura zitokanazo na ajali za barabarani, ili kuhakikisha kunakuwa na mwelekeo mmoja katika utoaji wa huduma na mawasiliano kwa umma.
“Wizara ya Afya tutaendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu matumizi salama ya barabara kwa kushirikiana na wizara nyingine, pamoja na kutumia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii ili kufikisha ujumbe kwa wananchi wote wa Tanzania,” amesisitiza.
Kwa upande wake, Mwakilishi na Mshauri wa Mradi wa JICA (Project Formulation Advisor), Bw. Sumi Yukiyasu, amesema tangu kuanza kwa mradi huo mwaka 2025 mafanikio makubwa yamepatikana kupitia ushirikiano na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji pamoja na Kikosi cha Usalama Barabarani cha Jeshi la Polisi, hususan katika maeneo yenye msongamano mkubwa wa watu kama Dar es Salaam.
Ameongeza kuwa JICA itaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania ili kuboresha huduma za dharura na kuimarisha usalama barabarani kwa manufaa ya wananchi.
Kufanyika kwa kikao hicho kumedhihirisha dhamira ya Tanzania na Japan ya kuendeleza ushirikiano katika kuelimisha jamii kuhusu matumizi salama ya barabara, kuboresha huduma za dharura na kupunguza vifo pamoja na madhara yanayosababishwa na ajali za barabarani nchini.
Kikao hicho kilifanyika katika Ofisi ya Mganga Mkuu wa Serikali kwa lengo la kutoa taarifa kuhusu maendeleo ya utekelezaji wa mradi wa Project for Road Safety Strengthening in Tanzania.