Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
CHAMA Cha Mapinduzi kimesema hakuna tamko la CCM na ACT bali ni tamko la mapatano ya kudumisha Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar kwa niaba ya Wananchi.
Pia, kimesisitiza tamko hilo kimsingi limezingatia kukuza Ustawi wa Kisiasa, Afya na maslahi ya pamoja katika kubeba dhima ya Maendeleo ya Wananchi.
Maelezo hayo yametamkwa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis, aliyesema tamko hilo ni matokeo kukamilika kwa mchakato wa mazungumzo baina ya CCM na ACT.
Mbeto akielezea kwa undani, alisema yaliomo ndani ya tamko hilo, yatasomwa kwa pamoja na pande zote za kisiasa huku wananchi na dunia ikishuhudia.
Alisema, ni bada ya juhudi za mazungumzo yaliyoongozwa na Marais Wastaafu Zanzibar na kuwashirikisha Viongozi Wakuu wa CCM na ACT , kwa dhamira ya kujenga na kuendeleza Umoja.
“Yote yaliomo katika tamko hilo yatasomwa kwa pamoja. Msingi wa tamko hilo ni kuendeleza Amani, Umoja wa Kitaifa, Mshikamano, Usawa, Haki na Maelewano,” alisema Mbeto.
Aidha, Katibu huyo Mwenezi aliwaeleza Waandishi wa habari waliofika Ofisini kwake, huku akilitaja tamko hilo, limezingatia kuweka namna bora ya kuipeleka mbele Zanzibar.
“Tumedhamiria kwa dhati kufanya kazi pamoja , kushirikiana na kusimamia maelewano. Mahali walipo watu wazima haliharibiki neno. Tuna matumaini kuliko wakati wowote,” alisisitiza Mbeto.
Hata hivyo, Mwenezi huyo wa CCM aliwataka wananchi wote wa Unguja na Pemba kulipokea tamko hilo, kulitegemea na kusimamia kwa madhumuni ya kuendeleza Umoja na Amani.