Na Hassan Kimweri, WAF – Morogoro
SERIKALI imedhamiria kuendelea kuboresha uhifadhi wa chanjo nchini kwa kuendeleza mifumo iliyoanzishwa kupitia mradi wa ‘Rapid Repair and Response (R3) wa usajili na usimamizi wa matengenezo ya majokofu ya chanjo na vifaa vya mnyororo baridi baada ya mradi huo kukamilika kwa kushirikiana na wadau wa ‘inSupply Health Tanzania’.
Hayo yamesemwa leo Juni 30, 2026 na Dkt. Florian Tinuga kutoka Idara ya Huduma za Afya, Kitengo cha Huduma za Kinga, Ofisi ya Rais – TAMISEMI wakati akifunga kikao kazi cha kujadili tathmini ya utekelezaji wa mradi huo baada ya kumalizika kwa muda wake.
“Mafanikio yaliyopatikana kupitia mradi huo yanapaswa kuendelezwa kwa kuhakikisha mifumo ya usimamizi wa matengenezo ya majokofu ya chanjo na vifaa vya mnyororo baridi inaendelea kufanya kazi kwa ufanisi katika ngazi zote za utoaji wa huduma za afya,” amesema Dkt. Tinuga
Aidha, Dkt. Tinuga amesisitiza kuwa wataalamu wa afya wanapaswa kuendelea kufuata miongozo na protokali za utekelezaji ili kuhakikisha halijoto inayohitajika kwa uhifadhi wa chanjo inadumishwa wakati wote, hatua itakayosaidia kulinda ubora wa chanjo na kuhakikisha wananchi wanaendelea kupata huduma salama na zenye viwango vinavyokubalika.
Pia, amewataka washiriki kutumia maarifa na uzoefu walioupata kupitia mradi wa R3 kwa kuboresha usimamizi wa vifaa vya mnyororo baridi pamoja na kushughulikia kwa wakati changamoto zinazoweza kujitokeza katika matengenezo ya vifaa hivyo.
“Lakini pia nisisitize umuhimu wa kuendelea kujenga uwezo wa watumishi wa afya, kuimarisha ufuatiliaji wa utendaji wa vifaa, kuboresha mfumo wa ukusanyaji na matumizi ya taarifa, pamoja na kuhakikisha miongozo ya utekelezaji inafuatwa ipasavyo katika ngazi zote,” amesema Dkt. Tinuga
Kwa upande wake, washiriki wa kikao hicho walieleza kuwa utekelezaji wa mradi wa R3 umechangia kuimarika kwa usimamizi wa matengenezo ya majokofu ya chanjo na vifaa vya mnyororo baridi, hatua iliyosaidia kuongeza ufanisi wa huduma za chanjo katika maeneo mbalimbali nchini.
Kikao kazi hicho kilitoa fursa kwa wataalamu kutathmini mafanikio, kujadili changamoto zilizojitokeza wakati wa utekelezaji wa mradi na kuweka mikakati ya kuhakikisha mafanikio yaliyopatikana yanaendelezwa kupitia usimamizi madhubuti, ufuatiliaji endelevu na ushirikiano kati ya wadau wa sekta ya afya.