Katibu wa Kamati Maalumu ya NEC Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis.
Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
KATIBU wa Kamati Maalum NEC Zanzibar Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo Khamis Mbeto Khamis amesema Chama cha Mapinduzi (CCM) hakipo tayari kuona Mtanzania yeyote akifa kwasababu ya kukosa matibabu kwenye hospitali zilizopo Bara na Visiwani.
Mbeto amesema hayo mbele ya waandishi wa habari wakati akifafanua madai yanayotolewa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu baadhi ya watu kukosa huduma za matibabu kwenye hospitali za mjini hapa.
Alisema, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar zimetenga bajeti kwa ajili ya Watanzania kupata matibabu, pia umewekwa utaratibu kwa wanaokwenda kupata huduma kwenye hospitali hizo, hivyo ni vema utaratibu ukafuatwa.
Alisema, upo utaratibu wa matibabu kupitia bima ya Afya na Matibabu kadi, ambazo zinamuwezesha Mtanzania kupata matibabu kwenye hospitali za Bara na Visiwani, hivyo ni vema kujiunga na huduma hizo ikizingatiwa Serikali imetoa fursa kwa taasisi za watu binafsi kutoa huduma za afya kwa kutumia kadi hizo, pia upo utaratibu wa kuchangia.
“Hakuna ubaguzi wowote, Mtanzania yeyote anatibiwa, hakuna ripoti yoyote inayosema kuna mtu amesema ametoka Bukoba hakutibiwa, hata sisi tunakwenda Muhimbili,” alisema na kuongeza kuwa, naye ni shuhuda suala hilo, kwani alimpeleka mtoto wake kupata matibabu ya mgongo kwenye hospitali ya Muhimbili Dar es Salaam, akaonyesha kadi akahudumiwa.
Alisema, suala hilo sio kubwa na halipaswi kuzua taharuki, kwani viongozi wote wanajua kwamba, imewekwa mifumo kutokana na bajeti ambazo zinatengwa “kwahiyo niseme kwamba, hiki chama ndo chenye Serikali zote mbili, hakuna Mtanzania yeyote atakayekosa matibabu,”
“Aidha uwe na kadi au hauna, hatuwezi kumuacha Mtanzania afe, lakini ni vema tukafuata utaratibu, kwa wale ambao hawastahili kupata matibabu kadi, ipo NHIF, wafuate taratibu ili kuepuka usumbufu. Sisi ni Watanzania na tutaendelea kuulinda U-Tanzania wetu.”