Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
KATIBU wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis amesema hivisasa Chama cha Mapinduzi (CCM) kipaumbele chake ni kuwatumikia watanzania waliowapa ridhaa kupitia Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 29, 2026.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mbeto alisema, Watanzania wanataka kuona barabara zinajengwa, elimu za watoto wao zinaimarishwa, na huduma nyingine za kijamii zinafanyika, na ndio kazi inayofanywa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Dkt. Hussein Mwinyi.
“Ndio maana mnawaona viongozi wetu wakuu wapo kwenye mambo ya msingi; utasikia wanaenda kutembelea kukagua ujenzi wa mradi fulani, kufungua ‘forum’ fulani ya uwekezaji, kuhimiza mikopo kwa watanzania wanyonge,” alisema Mbeto.
Aliendelea kusema kuwa, siku kadhaa zilizopita, Rais Samia alisikika akihimiza vijana ambao hawana dhamana ya kuweka kwenye taasisi za mikopo, wajengwe uwezo wa kuaminika ili wapewe mikopo. “Hiyo ndio kazi ya CCM kuwatumikia wananchi, haya maneno mengine ya mipasho, sisi hatuna muda nayo, sisi nchi hii tumepewa dhamana na Watanzania.”
Mbeto alisema, amewasikia viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wakivishutumu vyombo vya Ulinzi na Usalama na kuwashutumu watu mbalimbali, jambo ambalo haliwezi kuwasaidia kwenye harakati zao za kisiasa.
“Wameacha kazi ya kufanya siasa na kuwaaminisha watanzania kwamba sisi mkituchagua tutafanya vizuri zaidi, wanavishutumu vyombo vya Ulinzi na Usalama. Jeshi la Polisi lipo kwa mujibu wa Katiba, ibara ya 147, ibara hii ndio imeunda vyombo vya Ulinzi na Usalama,” alisema.
Alisema, Polisi wamepewa jukumu kwa mujibu wa sheria yao ya PGO (Police General Order), kusimamia usalama wa raia, kusimamia mali zao, kulinda kila kitu, hivyo hata kama wanasiasa wa upinzani hawalitaki Jeshi hilo, hawawezi kulikwepa, kwani hata shughuli zao ili zifanyike, zinahitaji kutolewa taarifa Polisi.
“Hivi vyombo vyetu vyote havina jema hata moja? Leo wanalala vizuri, wanaamka vizuri, wanafanya shughuli zao za kijamii vizuri, hivi vyombo vyote havina heri? Utawasikia wanasema wanaisaidia CCM, ni kweli wanatusaidia kutulindia mali zetu, na hili ni jukumu ambalo wanalifanya kwa watanzania wote,” alisisitiza Mbeto.
Mwenezi Mbeto alisema, kazi ya Jeshi la Polisi ni kuchunguza kama kuna viashiria vya uvunjifu wa amani na wakihisi kuna mtu anaweza kuwasaidia kukamilisha uchunguzi wao, au kusaidia hilo jambo ovu lisitokee, ni wajibu wao na hawana kosa, hivyo waachwe watimize majukumu yao.