Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
CHAMA cha Mapinduzi (CCM) kimesema, mvuto na kazi nzuri ya kuleta maendeleo inayofanywa na Rais wa Zanzibar Dkt. Hussein Mwinyi, imechangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la wanachama sambamba na hamasa ya kukiunga mkono chama hicho.
Hayo yamesema na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis alipozungumza na waandishi wa habari, ambapo alisema, suala la kuhamasisha wanachama lipo chini ya idara yao, hivyo wataendelea na jitihada hizo.
Mbeto alisema, wanafanyia kazi maagizo ya Rais Mwinyi ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, aliyoyatoa hivi karibuni wakati wa mikutano yake ya kuwashukuru wananchi na wanachama wa chama hicho kwa kuwapa ridhaa ya kuongoza kwa Awamu nyingine, kupitia uchaguzi uliofanyika Oktoba 29, 2025.
“Idara yetu tangu tumeingia, tumejitahidi kufanya hamasa na sidhani kama kuna kipindi yameibuka makundi mengi ya hamasa kama kipindi hiki, tumekuwa karibu na makundi hayo, tunawapa mashirikiano ya kuunda makundi haya, tutaendelea kufanya makongamano mbalimbali,”
“Tutaendelea kutoa mafunzo kama yalivyotolewa maelekezo na Makamu Mwenyekiti, tutaendelea kutoa mafunzo kwa makada na makundi haya, kuhakikisha hamasa ya CCM inakuwa kubwa,” alisema Mbeto.
Aliendelea kusema, “Kwenye Kisiwa cha Pemba wanachama wengi wamehamasika, wameipenda CCM, wameiunga mkono CCM, na wameendelea kushiriki kwenye mambo mbalimbali ya CCM kutokana na mvuto wa Dkt. Mwinyi na kazi nzuri iliyofanywa na Dkt. Mwinyi na WanaCCM kwa ujumla, bila kuisahau Idara hii ya Itikadi na Uenezi.”
Alisema, kwa nafasi yake ya Uenezi amekuwa akialikwa na makundi mbalimbali na anaitikia wito na watu wanaipenda CCM na wanahamasika, huku akisisitiza raha zitaendelea ndani ya Idara hii na ndani ya Chama cha Mapinduzi.”