OWM-TAMISEMI, Iringa
WASHIRIKI wa Mashindano ya Umoja wa Michezo na Taaluma Tanzania kwa Shule za Msingi (UMITASHUMTA) 2026 kutoka mikoa mbalimbali nchini wameanza kuwasili mkoani Iringa kwa ajili ya kushiriki mashindano hayo ya kitaifa yanayotarajiwa kuibua na kukuza vipaji vya michezo kwa watoto wa shule za msingi.
Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Uratibu wa Michezo, Utamaduni na Sanaa katika Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Yusuph Singo, amesema maandalizi ya mashindano hayo yamekamilika kwa kiwango cha kuridhisha na kwamba washiriki wanaendelea kuwasili na kupokelewa katika vituo vilivyotengwa.
“Washiriki wanaendelea kufika na kupokelewa kwa ajili ya hatua zinazofuata ili waweze kushiriki mashindano haya ambayo ni msingi muhimu wa kuibua na kuendeleza wanamichezo wa baadaye,” amesema Singo.
Kwa upande wake, Mratibu wa Michezo kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, George Mbijima, amesema maandalizi ya miundombinu na maeneo yote yatakayotumika kwa mashindano hayo yamekamilika kwa zaidi ya asilimia 90.
“Tupo katika hatua za mwisho za maandalizi. Viwanja vimeboreshwa, waamuzi, walimu na waratibu wa michezo mbalimbali wamewasili tayari kwa kuanza kazi. Tunaamini mashindano ya mwaka huu yatakuwa bora zaidi kuliko mwaka uliopita,” amesema Mbijima.
Naye Mratibu wa UMITASHUMTA Mkoa wa Mwanza, Joseph Mambo amesema mkoa huo ambao uliibuka bingwa wa jumla mwaka 2025 umejipanga kikamilifu kutetea ubingwa wake katika mashindano ya mwaka huu.
Mashindano hayo yanayowakutanisha wanamichezo kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara pamoja na Zanzibar, ikiwemo Unguja na Pemba, yanatarajiwa kufunguliwa rasmi Juni 9, 2026 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Profesa Riziki Shemdoe.
UMITASHUMTA na UMISSETA 2026 yanaandaliwa na kuratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo.
Mashindano hayo yanafanyika chini ya kaulimbiu isemayo: “Michezo na Sanaa Shuleni: Daraja la Ajira, Afya na Ushindani wa Kimataifa.”