RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Jukwaa la Uwekezaji Zanzibar 2026 limefanikiwa kuibua fursa mpya za uwekezaji, kuimarisha ushirikiano wa kimataifa na kuchochea ukuaji wa uchumi wa Zanzibar.
Akizungumza katika hafla ya Presidential Gala Dinner iliyofanyika Hoteli ya Diamond Bijoux, Bwejuu, Rais Dkt. Mwinyi amewahakikishia wawekezaji kuwa Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji kupitia uwazi, uwajibikaji na mageuzi ya sekta husika.
Aidha, ameipongeza Mamlaka ya Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) kwa kufanikisha jukwaa hilo lililowakutanisha washiriki zaidi ya 600 kutoka mataifa mbalimbali duniani, na kuitangaza Zanzibar kama kitovu cha uwekezaji chenye ushindani mkubwa.
Katika hafla hiyo, Rais Dkt. Mwinyi ametunukiwa Tuzo Maalum ya Uongozi katika Maendeleo ya Sekta ya Uwekezaji Zanzibar na ZIPA, kutambua mchango wake katika kuimarisha mazingira ya uwekezaji nchini.
Sambamba na hilo, Rais Dkt. Mwinyi amekutana na Watanzania wanaoishi nje ya nchi (Diaspora) na kuwahimiza kuwekeza Zanzibar pamoja na kuchangia maarifa na ujuzi wao katika maendeleo ya Taifa.