TANZANIA ni miongoni mwa nchi ambazo uchumi wake unakua kwa kasi duniani huku ikiendelea kudhibiti mfumuko wa bei, kuboresha mazingira ya uwekezaji na kuimarisha miundombinu ya mawasiliano pamoja na usafirishaji.
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Fedha, Mhandisi Mshamu Ali Munde alipokutana na kufanya mazungumzo na Uongozi wa Citibank, ukiongozwa na Mkuu wa Kanda ya Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara wa benki hiyo, Mustapha Akinsowon Dawodu, katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha, jijini Dar Es Salaam.
Alisema kuwa Tanzania inaendelea kuwa kitovu cha biashara na usambazaji wa vifaa mbalimbali kwa eneo la Afrika Mashariki ambacho pia kinaunga mkono matarajio ya ukuaji na mvuto wa Tanzania kama sehemu ya uwekezaji wa kigeni ili kuendelea kukuza uchumi wa nchi.
‘’Nchi hii inaendelea kufuata ajenda ya maendeleo ya kimkakati katika sekta muhimu, ikiwemo nishati, usafirishaji, kilimo, maji, na uzalishaji wa vifaa mbalimbali vinavyouzwa katika nchi mbalimbali ikiwemo nchi Wanachama, Jumuiya ya Afrika Mashariki,” alisema Mhandisi Munde.
Munde aliongeza kuwa katika Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050, Serikali imeweka mkazo kwa sekta binafsi kuchangia asilimia 70 kukuza uchumi hivyo ameisisitiza benki hiyo kuendelea kuwawezesha wawekezaji kukuza mitaji yao, lengo likiwa kuwaongezea hamasa ya kuwekeza zaidi katika maeneo ya kimakakati na yenye tija kwa Watanzania na taifa kwa ujumla.
Munde aliusihi Uongozi wa benki hiyo kuendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika nyanja mbalimbali ikiwemo kutekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati ili kuyafikia malengo yaliyowekwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
‘’Zaidi ya hayo, tunawaalika Citibank Tanzania Limited, kuzingatia kupanua ushirikiano wake na Tanzania zaidi ya mradi wa Uwanja wa Ndege wa Pemba, mchunguze maeneo mengine ya ushirikiano yanayolingana na malengo ya maendeleo ya kitaifa ya Tanzania na maslahi ya kimkakati ya Citibank,’’ alisema Munde.
Kwa Upande wake Mkuu wa Kanda ya Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara wa Citibank, Mustapha Akinsowon Dawodu, aliipongeza Serikali ya Tanzania inayoongozwa na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ya usafirishaji, pamoja na nishati huku benki hiyo ikiahidi kutoa ushirikiano kwa Tanzania.
‘’Tunaendelea kuangalia na kutafakari maeneo ambayo tutashirikiana na Tanzania, kama ambavyo tumekuwa tukifanya hivyo’’ alisema Dawodu.
Aliongeza kuwa Citibank imeendelea kuinadi Tanzania kwa wawekezaji wa nje kama nchi salama yenye mazingira mazuri ya uwekezaji kwa kuwa benki hiyo imekuwepo nchini kwa miaka takribani 31 hivyo inatambua umuhimu wa kuwekeza hapa nchini.