Na Albert Kawogo
BANDARI ya Dar es Salaam ni lango kuu la biashara kwa Tanzania na nchi jirani zisizo na bandari kama vile Zambia, Rwanda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Kwa muda mrefu, bandari hii imekuwa mhimili muhimu wa uchumi wa Taifa, lakini pia ilikabiliwa na changamoto za ucheleweshaji wa mizigo, msongamano wa makontena, na gharama kubwa za uendeshaji.
Katika jitihada za kuboresha ufanisi, Serikali ya Tanzania kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) mwaka 2023 iliingia ubia na kampuni ya kimataifa ya DP World ya Dubai.
Kupitia uwekezaji wa teknolojia za kisasa na mitambo ya hali ya juu, muda wa kushusha na kupakia mizigo umepungua kwa kiasi kikubwa. DP World imeleta uzoefu wake wa kimataifa katika usimamizi wa bandari, jambo lililosaidia kuongeza kasi ya mzunguko wa meli na kupunguza msongamano.

Hivi karibuni Wahariri kutoka vyombo mbalimbali vya habari walifanya ziara kutembelea Bandari ya Dar es Salaam na kupata fursa ya kujionea shughuli tofauti tofauti zinazofanywa DP World katika hatua za kuboresha ufanisi wa bandari hiyo.
Wahariri walishuhudia kwa kuona ni kwa namba gani ubia huo umechochea uwekezaji wa kisasa hasa katika mifumo ya kidigitali, ikiwemo matumizi ya mifumo ya kisasa ya ufuatiliaji wa mizigo.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Mahusiano wa DP World Elitunu Malamia anasema uwekezaji wao umeongeza uwazi, kupunguza makosa ya kibinadamu, na kurahisisha taratibu za kiforodha sambamba na kuongezeka kwa mapato ya serikali.
Malamia anasema kwa mujibu wa takwimu, makontena yanayohudumiwa yameongezeka kutoka 165,545 mwaka 2023 hadi 323,837 mwaka 2025 ambayo ni sawa na ukuaji wa asilimia 96.
Anafafanua kuwa mafanikio haya yametokana ufanisi mkubwa ulioweza kuvutia meli nyingi kufika kwa idadi kubwa bandari ya Dar es Salaam na hivyo mizigo kuongezeka.
“Kwa kuboresha ufanisi tumeweza kuvutia meli nyingi zaidi, mapato yatokanayo na shughuli za bandari yameongezeka na bandari sasa inahudumia mizigo mingi kwa muda mfupi zaidi, jambo linalochochea ukuaji wa biashara ya ndani na ya Kimataifa,”
anasema Malamia.
Anasema bandari ya Dar es Salaam sasa ina uwezo mkubwa wa kushindana na bandari nyingine katika ukanda wa Afrika Mashariki kama vile Bandari ya Mombasa.
Pia, afisa huyo anasema takwimu rasmi zinaonyesha ongezeko kubwa la mizigo ya jumla (general cargo) kutoka tani Milioni 1.22 mwaka 2023 hadi tani Milioni 2.23 mwaka 2025 ambao ni sawa na ukuaji wa asilimia 81.
Malamia anasema ongezeko hilo linaonyesha kuimarika kwa mnyororo wa usambazaji na kuongezeka kwa imani ya wafanyabiashara.
Aidha anasema maboresho ya ufanisi kwa bandari ya Dar es Salaam yameongeza mapato ya serikali kwa kasi kubwa ambapo makusanyo ya kila mwezi kupitia TRA yamepanda kutoka wastani wa Shilingi Milioni 800 hadi zaidi ya Shilingi Trilioni 1.
Pamoja na mafanikio haya makubwa kwa muda mfupi Malamia anasema kuna changamoto kubwa ya kutokuimarika kwa miundombinu ya barabara.
“Tumefanya maboresho makubwa yaliyochochea kuongezeka kwa meli na mizigo lakini barabara zetu ziko vile vile na hivyo kuchangia ugumu katika usafirishaji wa mizigo kutoka bandarini kwenda bandari kavu au nje ya nchi,” anasema Malamia.
Kwa ujumla, ubia kati ya TPA na DP World umeleta maboresho makubwa katika ufanisi wa huduma za Bandari ya Dar es Salaam. Ikiwa utaendelea kusimamiwa vizuri, ushirikiano huu unaweza kuwa chachu ya kukuza uchumi wa Tanzania na kuimarisha nafasi yake kama kitovu cha biashara katika Afrika Mashariki na Kati.