WAZIRI Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba ametangaza kuwa Serikali itaendelea kuongeza na kuboresha bajeti ya elimu sambamba na utekelezaji wa mtaala mpya, ili kufidia mahitaji yanayojitokeza shuleni na kuweka mazingira bora ya ujifunzaji.
Kauli hiyo imetolewa Bungeni jijini Dodoma katika kipindi cha maswali ya papo kwa papo, huku ikisisitizwa kuwa maboresho hayo yanalenga kumwezesha kila mtoto kusoma bila vikwazo.
“Kwa kuwa tunaenda katika mtaala mpya wa elimu, tutaendelea kuboresha bajeti. Tutaendelea kuboresha bajeti kwa sababu mahitaji yanaongezeka kila wakati katika kumfanya mtoto asome vizuri,” amesema Mwigulu.
Akijibu hoja ya Mbunge wa Segerea kuhusu michango holela shuleni, Waziri Mkuu ameeleza kuwa Serikali inatambua na kukubali utaratibu wa michango ya chakula iliyozoeleka, lakini amesisitiza kuwa michango mingine yoyote lazima izingatie miongozo ya Serikali na kupata idhini ya Wakuu wa Mikoa ili kuepusha uonevu na usumbufu kwa wazazi na wanafunzi.
Katika kufafanua msimamo wa Serikali dhidi ya michango isiyo halali, Waziri Mkuu amerejea tukio la mwanafunzi aliyedaiwa shilingi 50,000 za dawati mkoani Katavi na kuzuiwa kujiunga na sekondari.
Serikali iliamuru mtoto arejeshwe darasani mara moja na vyombo vya nidhamu vichukue hatua kwa uongozi wa shule uliosababisha mwanafunzi kukosa masomo kwa miezi kadhaa.