Na Shaban K. Juma, WAF – Dar es Salaam
SERIKALI imepongeza Hospitali ya E.M ya Kigamboni kwa kuwekeza takribani Shilingi Bilioni 10 katika kuboresha huduma za afya, wakati wa uzinduzi rasmi huduma za kisasa za uchujaji damu (dialysis) pamoja na CT Scan, hatua itakayorahisisha upatikanaji wa huduma hizo kwa wananchi.
Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi, ametoa pongezi hizo Machi 27, 2026 jijini Dar es Salaam akimwakilisha Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa, katika hafla ya uzinduzi huo.
Amesema uwekezaji huo unaimarisha mchango wa sekta binafsi kwenye kuboresha huduma za afya na kusogeza huduma za kibingwa karibu na wananchi.
Dkt. Samizi ameeleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuweka mazingira rafiki kwa wawekezaji kushirikiana na Serikali na kuendeleza sekta ya afya.
Serikali imeimarisha miundombinu, imenunua vifaa tiba vya kisasa na imeongeza wataalamu ili kuboresha huduma hizo.
Amesisitiza kuwa uwekezaji huo unaonesha dhamira ya pamoja ya kuokoa maisha ya Watanzania na kuongeza kuwa, Serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora kwa urahisi na gharama nafuu.
Dkt. Samizi amebainisha kuwa huduma za dialysis zinasaidia wagonjwa wa figo, huku CT Scan ikiwezesha wataalamu kugundua magonjwa kwa haraka na usahihi zaidi, hivyo kuharakisha matibabu.
Amesema kwa sasa vituo 74 nchini vinatoa huduma za dialysis, na zaidi ya nusu vinamilikiwa na sekta binafsi, jambo linaloonyesha umuhimu wa sekta hiyo kwa maendeleo ya afya.
Aidha, uzinduzi wa huduma hizo katika Hospitali ya E.M utawasaidia wakazi wa Kigamboni na maeneo jirani kupata huduma karibu zaidi, kupunguza gharama za matibabu na kuokoa muda.
Katika hatua nyingine, Dkt. Samizi ameeleza kuwa magonjwa yasiyoambukiza yanachangia asilimia 33 ya vifo nchini, huku akihimiza wananchi kubadili mtindo wa maisha, kufanya uchunguzi wa afya mara kwa mara na kuepuka matumizi holela ya dawa.