WAZIRI Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba amewaomba Watanzania waendelee kumuombea kwa Mwenyezi Mungu aliyekuwa Waziri Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, marehemu William Lukuvi aliyefariki jana Machi 25, 2026 katika Hospitali ya Benjamin Mkapa, jijini Dodoma.
Akiongea kwa niaba ya Serikali nyumbani kwa marehemu Area D, jijini Dodoma leo, Alhamisi, Machi 26, 2026, Waziri Mkuu amesema: “Kwa niaba ya Serikali natoa pole kwa familia, ndugu, jamaa. Jambo hili zito, gumu kulielewa, gumu kulipokea.”
…Lakini ndio limeshatufika na sote hatukutarajia maana Mheshimiwa Waziri alikuwa kazini. Tuendelee kumuombea kwa Mwenyezi Mungu na kuifariji familia. Mwenyezi Mungu awaimarishe kwa sababu yeyé ndio mfariji mkuu,” amesisitiza.
Vilevile, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu ametumia fursa hiyo kuihakikishia familia kwamba Serikali itaendelea kuwa pamoja nayo katika kipindi hiki chote cha majonzi.
Viongozi wengine waliokuwepo msibani hapo ni pamoja na Naibu Spika, Daniel Siro, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Masauni, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumisi wa Umma na Utawala Bora), Ridhiwani Kikwete, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule na Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha, Dkt. Toba Nguvila.