Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), Mhandisi Peter Mwasalyanda
WANANCHI wa maeneo ya vijijini nchini, wanaokadiriwa kufikia takribani milioni 2.7, wanatarajiwa kunufaika na huduma bora za mawasiliano kufuatia utekelezaji wa Mradi wa Ujenzi wa Minara ya Mawasiliano ya Simu Awamu ya Kumi (10).
Mikataba ya mradi huo imesainiwa hivi karibuni kati ya Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) na makampuni ya mawasiliano ya simu.
Kupitia mradi huo, jumla ya minara 201 itajengwa katika kata 201 zenye vijiji 263, hususan katika maeneo ya vijijini ambayo awali yalikuwa hayana au yalikuwa na huduma hafifu za mawasiliano. Ujenzi wa minara hiyo unalenga kuongeza upatikanaji wa huduma za uhakika za simu na intaneti kwa wananchi.