Na Mwandishi wetu, Zanzibar
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesikitishwa na matamshi yanayoendelea kutamkwa na Viongozi wawili wa ACT Wazalendo wanaotumia Siasa za Ubaguzi, Ukabila na Asili za watu kama Sera za chama hicho.
Imetajwa aina ya Siasa, Mahubiri na Sera hizo ni hatari kwa Ustawi wa Maisha ya Jamii na Mustakabali wa Usalama wa Taifa.
Matamshi hayo yametamkwa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis aliyewataja Makamu Mwenyekiti wa ACT Ismail Jussa Ladhu na Mgombea Urais Othman Masoud Othman (OMO) ni virusi hatari kwa umoja Zanzibar.
Mbeto alisema, Jussa na OMO ni Wanasiasa waumini wa Sera na Siasa za kibaguzi Zanzibar wakitumia kama mtaji wa kisiasa wakitaka wakubalike katika jamii.
Alisema, wanasiasa hao wana ajenda ya kuirudisha Zanzibar katika zama za Ukoloni uliowaweka watu katika makundi na mitazamo ya matabaka ya Rangi, Asili na Ukabila.
“ACT kimeshindwa kutaja sera zake mbele ya Wananchi, hivyo kimeamua kupandikiza Chuki, Ukabila na kutaja Asili za watu. Ni Jussa na OMO wanaotaka kuipasua jamii,” alieleza Mbeto.
Katibu huyo Mwenezi aliongeza, ili nchi iwe na Utaifa lazima kuwe na Amani, Umoja na Mshikamano, lakini chini ya mpango mkakati huo, ACT, kimekusudia kuigawa jamii.
“CCM kinalaani matamshi ya viongozi hao kwa sauti ya juu. Ubaguzi, Ukabila na kutaja Asili za watu ni hatari katika jamii. Othman na Jussa wameshindwa kuwashawishi wananchi kwa hoja na sera,” alieleza Mbeto.
Katibu huyo Mwenezi alisema, Siasa au Sera za Ukabila, Rangi za watu na Asili ni kwenda kinyume na Sheria Namba 5 ya Mwaka 1992 ya Usajili wa Vyama vya Siasa nchini.
Mbeto alisema, Sheria hiyo inapiga marufuku Vyama kujihusisha na Sera za ukabila, kutumia alama au majina ya vyama vya zamani na aina yoyote ya Ubaguzi.
“Tunalaani kuwasikia ACT wakiwabagua wenzao kwa nasaba na ukabila. Kinachoendelea katika majukwaa ya kampeni ya ACT ni kuiyumbisha jamii na kupandikiza chuki,” alifafanua Mbeto.
Hata hivyo, CCM kimeyaita matamshi hayo hayana dhamira njema, ingawaje wananchi wamewashtukia viongozi wa chama hicho kutaka kuirudisha tena Zanzibar katika misukosuko.