MGOMBEA wa nafasi ya Rais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Serikali itaendelea kujenga masoko katika kila wilaya na mkoa ili kuandaa mazingira bora zaidi kwa wajasiriamali nchini.
Akizungumza na makundi mbalimbali ya Wajasiriamali, waendesha bodaboda na bajaji, Wajane, Wavuvi na Wakulima katika mkutano wa hadhara wa kampeni uliofanyika katika Uwanja wa Michezo wa Kihinani, Mkoa wa Mjini Magharibi leo Oktoba 18, 2025, Dkt. Mwinyi amesema hatua hiyo inalenga kuwawezesha wajasiriamali kufanya biashara katika mazingira salama, ya kisasa, na yenye tija.
Halikadhalika, Dkt.Mwinyi ameeleza kuwa Serikali itaendelea kuwapatia wajasiriamali mafunzo ya biashara na alama za ubora ili bidhaa zao ziweze kufikia viwango vya kimataifa na kuhimili ushindani wa soko la kikanda na kimataifa.
Kuhusu tozo za masoko, Dkt. Mwinyi amesema Serikali italifanyia kazi suala hilo kwa lengo la kuhakikisha wajasiriamali wanatozwa viwango rafiki vinavyorahisisha shughuli zao za kila siku.
Aidha, aliahidi kujenga vituo vya mabasi vyenye maeneo maalum kwa bodaboda, na kutoa mikopo nafuu kwa wajasiriamali baada ya kurasimisha biashara zao.
Katika sekta ya kilimo, Dkt. Mwinyi amebainisha kuwa Serikali itaendelea kuimarisha skimu za umwagiliaji, kuwapatia wakulima pembejeo, mbolea za bei nafuu, na mafunzo kupitia mabwana shamba ili kuongeza uzalishaji na kujitosheleza kwa chakula.
Kwa upande wa uvuvi, amesema Serikali itaendeleza ujenzi wa masoko ya kisasa na madiko, pamoja na viwanda vya kusarifu samaki katika eneo la Fungu Refu kwa lengo la kuongeza thamani ya mazao ya baharini, sambamba na ujenzi wa gati jipya katika eneo la Kihinani.
Akizungumzia masuala ya kijamii, Dkt. Mwinyi amesema Serikali itaweka adhabu kali kwa wazazi wanaotelekeza watoto wao ili kukomesha tabia hiyo, na ameahidi kuwawezesha wajane kupitia mikopo isiyo na riba na mafunzo ya kujikwamua kiuchumi.