Dkt. Mwinyi aahidi ujenzi wa barabara na gati Kisiwa cha Tumbatu

0

MGOMBEA Urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ameahidi kujenga gati ili wananchi wa kijiji cha Tumbatu kuondokana na usumbufu unaojitokeza katika kufuata huduma nje ya kisiwa chao kwa wakati.

Akizungumza na wanachama wa CCM na wananchi wa Jimbo la Tumbatu kwenye mkutano uliofanyika katika kiwanja cha mpira cha Tumbatu Uvuvini alisema, gati hilo litakapokamilika wananchi wataweza kupata huduma kwa urahisi.

Pia, amewaahidi kuwakamilishia miundombinu ya barabara itakayowasaidia kurahisisha kazi zao za kila siku.

Aidha alisema, Chama cha Mapinduzi, kimejidhatiti kuhakikisha kuwa wanatekeleza ajenda kuu ya kuona amani, utulivu na mshikamano unaendelea kudumu.

Hivyo, aliwasisitiza wananchi hao kutoruhusu mtu yoyote kuwabagua kwani ubaguzi hauwezi kuleta maendeleo katika nchi.

Alisema, vyama vingine vimekuwa vikihubiri masuala yaliyokuwa sio ya amani jambo ambalo hawapaswi kuwafuata na kuwasisitiza kuendeleza amani, mshikamano na maelewano yaliyokuwepo nchini.

Hata hivyo, alisema katika awamu ya pili endapo akichaguliwa atahakikisha anajenga skuli zenye hadhi na lengo kuona wanafunzi wote wanaingia katika shifti moja ili waweze kusoma elimu ya dini.

Akizungumzia suala la huduma za Afya, Dkt. Mwinyi, alisema katika hospitali iliyopo katika kisiwa hicho, ataleta dhana ikiwemo vifaa tiba vyenye hadhi ili wananchi wa kisiwa hicho waweze kupata huduma zilizokuwa bora.

Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dkt. Mohamed Said Mohamed Dimwa, alisema Dkt. Mwinyi, amekibadilisha kisiwa cha Zanzibar na Tumbatu kwa ujumla.

Alisema, wananchi wakikichagua Chama cha Mapinduzi ndio wamechagua maendeleo yako na wananchi kwa ujumla.

Aidha alisema, Dkt. Mwinyi yupo tayari kuwatumikia wananchi wote na ndio kiongozi anayependa kazi na lengo lake ni kuwatumikia wananchi wote wa Zanzibar.

Hivyo, aliwataka wazanzibar kuwachagua kwa kura za kishindo wakati ukifika ili maendeleo yaendelee kuwepo katika visiwa vya Zanzibar.

Nae, Katibu Mwenezi na mafunzo Zanzibar, Khamis Mbeto, alisema Dkt. Mwinyi ameviheshimisha visiwa vyote ikiwemo kisiwa cha uzi ng’ambwa ambapo ujenzi wa daraja unaendelea na kisiwa cha Tumbatu kimekuwa na maendeleo ikiwemo ujenzi wa skuli ya ghorofa.

Mohamed Omar, mkaazi wa Tumbatu, alisema wananchi wa Tumbatu hawana budi kumshukuru Dkt. Mwinyi na kumpongeza kwani amefanya mafanikio mengi katika kijiji hicho.

Alisema, katika kijiji hicho ipo skuli ya ghorofa, ujenzi wa hospitali ya wilaya, ambapo kwa Tumbatu mambo hayo yalikuwa mageni.

Sambamba na hayo, alisema limejengwa tenki kubwa la maji ambalo litawasaidia katika upatikanaji wa huduma za maji safi na salama, hivyo matumaini yake atapewa miaka mitano tena ili huduma hizo ziendelee.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here