Mbeto amtaja Rais Dkt. Mwinyi ni ramani ya maendeleo Zbar

0

Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimemtaja Mgombea wake wa Urais Rais Dkt. Huseein Ali Mwinyi kuwa ni dira na ramani iliofikisha Zanzibar katika Uwanja mpana wa maendeleo.

Kadhalika chama hicho, kimesifu juhudi na utendaji wa SMZ na jina la Dkt. Mwinyi limeingia katika rekodi ya utumishi uliotukuka.

Matamshi hayo yametamkwa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis aliyesema Zanzibar ya Mwaka 2025 kimaendeleo si ya Mwaka 2020.

Mbeto alisifu utendaji wa pamoja wa SMZ na kuitaja miradi mikubwa ya kisekta ilioanzishwa na kukamilika, hivyo maendeleo yaliopatikana yatabaki kuwa alama isiofutika.

Alisema, kutokana na utendaji wa serikali ya Awamu ya Nane, Rais Dk Mwinyi amefuata nyayo na urithi na matunda ya watangulizi wake katika kusimamia maendeleo ya nchi na watu.

“Rais Dkt. Mwinyi atabaki kuwa mfano na kielelezo cha utumishi bora. Miaka mitano ya serikali yake ametimiza wajibu kwa wananchi na kufanya mageuzi makubwa katika ustawi wa jamii,” alisema Mbeto.

Aidha, Katibu huyo Mwenezi alisema licha ya uongozi wa Rais Dkt. Mwinyi kuwa kama dira na ramani iliofikisha mbali Zanzibar kimaendeleo, lakini amewafanya wananchi waishi kwa upendo na umoja.

“Serikali ya Awamu ya Nane Zanzibar imekomesha maonevu, ubaguzi na upendeleo. Rais Dkt. Mwinyi amekataa kuongoza kwa hasama na chuki. Serikali yake imewajibika na kutumikia Wananchi,” alisisitiza.

Pia, Mbeto alisema, hakuna jambo lolote litakalomzuia asirudi tena ikulu, kwani aliyoyaahidi ameyatekeleza ikiwemo kuondosha changamoto alizozikuta na kufanikisha miradi ya kisekta.

“Wananchi ili kumtuza Rais Dkt. Mwinyi wameahidi kumpigia kura nyingi ili akamilishe kazi alioianza mwaka 2020. Mgombea Urais wa CCM hana deni kwa wananchi wake,” alisema Katibu huyo Mwenezi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here