WANANCHI na Wafanyabiashara wa Soko la Kibandamaiti Zanzibar wameelezea kuridhishwa kwao na maamuzi ya Serikali kuwajengea Soko la kisasa kwa lengo la kumaliza changamozo zinazowakabili.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti baada ya Mgombea Urais wa Zanzibar ambaye pia ni Rais wa Zanzibar Dkt. Hussein Mwinyi kumaliza hotuba yake ya Kampeni katika viunga vya soko hilo, wamesema ujenzi wa Soko hilo umekuja wakati sahihi kutokana na kukabiliwa changamoto mbali mbali za miundombinu duni katika Soko hilo.
Mfanyabishara wa matunda Juma Issa Suweid alisema, “Nimefurahi kusikia Serikali itaanza ujenzi wa Soko letu kuwa la kisasa, hatua hii inaleta faraja kubwa kwetu kwani itamaliza kero zote zinazotukabiri hapa Sokoni ambapo tutafanya biashara katika salama zaidi,”
Kwa upande wake Mama Lishe Zuwena Rajab, amepongeza hotuba ya Mgombea Urais wa Zanzibar Dkt. Hussein Mwinyi ambapo alisema, imebeba matumaini ya utatuzi wa changamoto za muda mrefu za wafanyabiashara hao.
Akitaja baadhi ya changamoto hizo alisema ni kujaa maji wakati wa msimu wa mvua, sambamba na ukosefu wa miundombinu ya kisasa ya kuhifadhi vyakula na bidhaa mbali mbali zinazouzwa sokoni hapo.
Akiwahutubia Wafanyabiashara na Wananchi hao, Mgombea nafasi ya Urais wa Zanzibar kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Mwinyi amesema Serikali inatarajia kujenga soko la kisasa Kibandamaiti.
Kauli hiyo ameitoa leo Septemba 30,2025 wakati akizungumza na wananchi na wafanyabiashara wa Kibandamaiti kwenye uwanja wa Kibandamaiti uliopo wilaya ya Mjini Zanzibar.
“Wakati tukijenga kituo cha Daladala Kijangwani,tuliwaomba muwe hapa kwa muda huku tukitafuta ufumbuzi wa kukujengeeni Soko la Kisasa ambapo kwa sasa muda wowote ujenzi wake utaanza,” alisema Dk Mwinyi.
Dkt. Mwinyi amesema, mchoro wa ujenzi wa soko hilo tayari na kwamba fedha zipo kipindi kifupi anatarajia kuanza ujenzi huo wa kisasa.
Kupitia ahadi yake hiyo aliwaomba Wafanyabiashara hao, kumchagua Dkt.Samia Suluhu Hassan kuwa Rais wa Tanzania, kumchagua Dkt. Mwinyi kuwa Rais wa Zanzibar pamoja na Wabunge, Wawakilishi na Madiwani wote wa CCM ili waendelee kutekeleza aahadi na maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2025/2030 kwa vitendo
Mapema, Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Dkt. Mohamed Said Mohammed Dimwa amesema, mgombea nafasi ya Urais wa Zanzibar kupitia CCM, Dkt. Mwinyi ni kiongozi mtendaji mahiri na mwenye uwezo wa kuifikisha Zanzibar kuwa nchi ya visiwa yenye maendeleo endelevu.
Amesema, Dkt. Mwinyi mara nyingi kazi zake zinaonekana kwa macho na kwamba zinapimika na zinasemwa na kila mtu.
Katika maelekezo yake Dkt. Dimwa amewaomba Wafanyabiashara hao kuendelea kumuamini Dkt. Mwinyi, na kwamba wampatie nafasi ya kumchagua kwa kura nyingi ili alete maendeleo endelevu.