RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema fani ya ubunifu wa majengo ni miongoni mwa sekta muhimu zinazochangia kuimarisha uchumi unaokua kwa kasi kila siku.
Dkt. Mwinyi aliyasema hayo Septemba 8, 2025, Ikulu Zanzibar, alipokutana na timu ya wabunifu wa majengo kutoka Taasisi ya Ubunifu wa Majengo ya Afrika Mashariki, wakiongozwa na Rais wa Taasisi hiyo, Mhandisi Mecky Tchawi.

Rais Dkt. Mwinyi aliihakikishia timu hiyo kuwa Zanzibar imeanza kuchukua hatua za kuanzisha kitivu cha taaluma ya ubunifu wa majengo katika vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu, kutokana na umuhimu wake katika ukuaji wa uchumi na ongezeko la miradi ya ujenzi katika sekta mbalimbali za maendeleo.
Aidha, alibainisha kuwa Serikali, kwa kushirikiana na taasisi hiyo, itatafuta mbinu muafaka za kufanikisha utekelezaji wa wazo hilo.
Katika mazungumzo hayo, Rais Dkt. Mwinyi pia ameridhia ombi la taasisi hiyo la kuwa mlezi wa kwanza mzawa wa Afrika Mashariki tangu kuanzishwa kwake mwaka 1913, na kukabidhiwa cheti maalum pamoja na kitabu cha historia ya taasisi hiyo.

Kwa upande wake, Rais wa Taasisi, Mhandisi Mecky Tchawi, alisema kasi ya ujenzi wa majengo katika nchi yoyote ni kielelezo cha ukuaji wa uchumi wake.
Alisisitiza kuwa, Zanzibar inapaswa kuwa na kitivu cha taaluma ya ubunifu wa majengo ili kuandaa wabunifu vijana wenye ujuzi na weledi wa kisasa.