Mbeto: Hakuna sababu za kutokuchaguliwa Rais Samia na Dkt. Mwinyi

0

Na Mwandishi Wetu

CHAMA cha Mapinduzi (CCM), kimejinasibu kuwa hakuna sababu ya Watanzania kutokuwapigia kura Rais Samia Suluhu Hassan na Dkt. Hussein Ali Mwinyi katika Uchaguzi Mkuu Oktoba mwaka huu 2025.

Akizungumza na wanahabari katika ukumbi wa CCM Kisiwandui, Zanzibar Agosti 27, 2025, Katibu wa Kamati Maalum NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo Khamis Mbeto Khamis alisema CCM kina matumaini makubwa na wagombea wao.

Chama hicho kimempitisha Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwania nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Rais Zanzibar.

Mbeto alisema, wote wawili wamefanya mambo makubwa ambayo hayawezi kuwafanya watanzania wakawanyima kura.

“Mama Samia amefanyakazi kubwa sana, nani asiyejua? Zamani tulikuwa tunaenda Dodoma saa 12 hadi 13, leo saa nne tu umefika, kuna haja ya kumchagua Mzee wa Ubwabwa au yule mwingine, anazunguka tu..!” alisema Mbeto.

Mwenezi huyo alibainisha kuwa Ilani ya uchaguzi Zanzibar, ilimtaka Rais Dkt. Mwinyi kujenga madarasa 1,500 yeye kajenga madarasa 5,000 na katakiwa shule 10, kajenga 61 sasa hapo wamnyime kura kwa nini.

“Wakati Ilani ya CCM, ilimtaka ajenge hospitali 4 yeye kajenga 61 wakati miundombinu ya barabara Ilani ilitaja Kilometa 196 lakini kaitekeleza na kuvuka na kujenga kilometa 1,000” alisema.

Mwenezi Mbeto alisema, Rais Mwinyi amegusa kila sekta wakiwemo wazee ambao posho yao imepandishwa kwa asilimia 150 kwani awali walilipwa Shilingi 20,000 lakini sasa ni Shilingi 100,000.

Wazee hao ni tofauti na wale wanaotunzwa na serikali ambao kwa mwezi wanapewa 40,000 kawaongeza 50,000 ikiwa ni pamoja na kula, kulala bure na gari la kutembelea limenunuliwa.

“Rais Mwinyi kawatoa kwenye masoko ya kuezekwa na mapolo mekundu (viroba) na kuwaleta katika masoko ya kisasa, soko la nyota tano kama Mwanakwelekwe, leo kuna wa kumnyima Dkt. Mwinyi..? ” alihoji.

Ujenzi wa barabara za lami mitaani ni jambo jingine la maendeleo ambalo awali halikuwepo.

“Ndio maana nasema na leo narudia tena, kazi yetu kumnadi Dkt. Mwinyi itakuwa rahisi maana alichokifanya kila mtu anakiona,” alisema mwenezi Mbeto.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here