MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango amesema zama za utandawazi zinayataka Mashirika ya Umma, Taasisi na Wakala za Serikali kuendelea kutoa huduma mbalimbali hata nje ya mipaka ya nchi.
Makamu wa Rais amesema hayo wakati akifungua Kikao Kazi cha Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Mashirika na Taasisi za Umma kinachofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Arusha (AICC).
Amewahimiza Wenyeviti wa bodi na Watendaji wakuu wa Mashirika ya umma, kuhakikisha wanatoa uongozi na mwelekeo wa Mashirika ili yaweze kutimiza wajibu wake kwa wananchi, ambao ndio wana hisa wake wakubwa.
Alisema, ni muhimu kujenga ushirikiano ili kuvutia uwekezaji, kukuza biashara na kuongeza nafasi za ajira kwa wananchi.
Ameongeza, kwamba Taasisi na Mashirika ya Umma hayana budi kuwa daraja baina ya Taifa na dunia ili kuhakikisha Tanzania inatambulika kimataifa, kama nchi yenye mazingira bora ya biashara na uwekezaji, ikiwa ni pamoja na kuchangamkia fursa za uwekezaji nje ya mipaka.
Pia, alisema ni vema kuimarisha ubora wa huduma pamoja na kuwa wabunifu na kuendana na kasi ya mabadiliko.
Halikadhalika, Makamu wa Rais amesisitiza umuhimu wa kulinda rasilimali zilizopo ambazo ni nyenzo muhimu katika kufikia azma ya kujenga mazingira ya ushindani.
Ametoa wito kwa Taasisi na Mashirika ya umma kuimarisha usimamizi wa matumizi ya fedha, kudhibiti manunuzi na kuimarisha usimamizi wa mikataba pamoja na kusimamia vema rasilimali watu.
Vilevile, Makamu wa Rais alisema ni muhimu kujenga ushirikiano wa kitaasisi kati ya Mashirika ya nchini na yale ya Kimataifa, ili kunufaika na masoko, teknolojia, tafiti na hata utamaduni wa kufanya kazi.
Pia, alisema ili kufikia malengo ni vema kuongeza bidii na weledi katika kazi ikiwa ni pamoja na ubunifu na ustadi katika uzalishaji na utoaji huduma mbalimbali.
Amewasihi Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu kusimamia weledi katika kazi na kuimarisha suala la utafiti kwa maendeleo ya nchi.