RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amewahakikishia walimu kuwa Serikali itaendelea kuimarisha maslahi na mazingira ya ufundishaji na kujifunza kwa dhamira ya kuboresha elimu zaidi.
Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, Agosti 12, 2025, katika kongamano la kumpongeza lililoandaliwa na Shirikisho la Walimu Zanzibar kufuatia mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya elimu nchini katika kipindi cha uongozi wake. Hafla hiyo imefanyika katika Ukumbi wa Dkt. Ali Mohamed Shein, Tunguu, Mkoa wa Kusini Unguja.
Aidha, Rais Dkt. Mwinyi alisema katika kuongeza motisha kwa walimu, Serikali imeboresha maslahi yao kwa kuongeza mishahara, posho za likizo na ufiwa, pamoja na kulipa malimbikizo mengine.
Halikadhalika, Rais Dkt.Mwinyi alisema Serikali imeajiri walimu wapya 5,265 na kuwapatia mafunzo mbalimbali ili kuongeza ufanisi wao.
Ameeleza kuwa kiasi cha Shilingi Bilioni 1.8 kimetumika katika mwaka wa fedha 2024/2025 kwa malipo ya rambirambi kwa wafiwa, pamoja na posho za walimu wakuu na wasaidizi wao, ikiwemo nyongeza ya posho za madaraka.
Aidha, Serikali imetenga Shilingi Bilioni 1.6 kwa malipo ya walimu wakuu na wasaidizi wao kwa mwaka wa fedha 2025/2026.
Rais Dkt. Mwinyi amefahamisha kuwa Serikali imeongeza bajeti ya sekta ya elimu kutoka Shilingi Bilioni 265 hadi kufikia Bilioni 864.
Kwa upande mwingine, Rais Dkt. Mwinyi ameongeza kuwa Serikali imeamua kukirejesha Chuo cha Ualimu cha Nkrumah kufuatia ombi la walimu, kutokana na kazi nzuri iliyokuwa ikifanywa na chuo hicho, ili kiendelee kuzalisha walimu bora na wenye sifa za ufundishaji.
Vilevile, Serikali imeanzisha Tume ya Walimu itakayoshughulikia changamoto zinazowakabili walimu.