Wenyeviti, wajumbe Mabaraza ya Kata Kibaha DC watakiwa kuzingatia maadili

0

HALMASHAURI ya Wilaya ya Kibaha kupitia Idara ya Sheria imeendesha mafunzo ya siku moja kwa Wenyeviti na Wajumbe wa Mabaraza ya Kata yaliyoko ndani ya Mamlaka ya Mji Mdogo wa Mlandizi, Juni 27, 2025.

Mafunzo hayo yalifunguliwa rasmi na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Wakili Emmanuel Mkwe, ambaye aliwataka washiriki kujikita zaidi katika kutatua migogoro kwa njia ya suluhu badala ya kutoa hukumu.

Alieleza kuwa Mabaraza ya Kata ni vyombo muhimu vya kutatua migogoro kwa mujibu wa Sheria ya Mabaraza ya Kata Sura 206, Toleo la Mwaka 2002.

“Tuwe sehemu ya utatuzi wa migogoro katika jamii kwa kutumia hekima, busara na sheria, na siyo chanzo cha migogoro. Hii ni sehemu ya kumsaidia Mheshimiwa Rais katika jitihada zake za kuhakikisha amani na mshikamano wa Kitaifa,” alisema Wakili Mkwe wakati wa kufunga mafunzo hayo.

Kwa upande wake, Mwanasheria wa Halmashauri Winfrida Kalua alisema lengo la mafunzo ni kuwawezesha wajumbe kuandaa na kuwasilisha taarifa kwa usahihi, sambamba na kuwajengea uwezo wa kushughulikia migogoro kwa kuzingatia taratibu za kisheria.

Wakufunzi wa mafunzo hayo walikuwa maofisa sheria wa Halmashauri ambao ni Yasmini Makanya, Peter Mundo na Fatma Rusimba. Walisisitiza wajumbe kuacha maslahi binafsi na kuzingatia maadili, kuepuka mgongano wa kimaslahi na kuwa waadilifu wakati wa usuluhishi wa migogoro.

Miongoni mwa washiriki wa mafunzo hayo ni Khadija Maarifa kutoka Kata ya Kawawa na George Kibwana kutoka Kata ya Kilangalanga ambao kwa nyakati tofauti walieleza kuwa wamepata uelewa mkubwa na wataenda kuyatekeleza mafunzo kwa vitendo ili kuleta amani na utulivu katika maeneo yao.

Mafunzo haya ni sehemu ya juhudi endelevu za Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha katika kuhakikisha kuwa vyombo vya usuluhishi katika ngazi ya jamii vinafanya kazi kwa ufanisi na kwa mujibu wa sheria.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here