NAIBU Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais -TAMISEMI anayeshughulikia Miundombinu, Mhandisi Rogatus Mativila amesema Ofisi ya Rais – TAMISEMI inatekeleza miradi mbalimbali yenye lengo la kuboresha miji nchini.
Miradi hiyo ni pamoja na DMDP, Uendelezaji wa Bonde la Mto Msimbazi jijini Dar es Salaam na mradi wa TACTIC unaotekelezwa katika miji 45 na kuongeza kuwa utiaji saini wa mikataba 12 ya miji 11 inayotekeleza mradi wa TACTIC ni muendelezo wa utekelezaji wa mradi huo.
Mhandisi Mativila amebainisha kuwa mpaka sasa majiji na miji 12 ya fungu la kwanza imeshatia saini mikataba mingine mwezi Septemba, 2023 jijini Dar es Salaam.
Majiji na miji hiyo ni pamoja na Mbeya, Arusha na Manispaa za Geita, Singida, Tabora, Kahama, Sumbawanga na Kigoma.
Hayo ameyasema wakati wa hafla ya utiaji saini wa mikataba 12 ya miji 11 iliyofanyika jijini Dodoma hivi karibuni.