Tudumishe amani yetu – DC. Ngubiagai

0

MKUU wa Wilaya ya Ukerewe, Mkoani Mwanza, Christopher Ngubiagai amewaasa wananchi kuendelea kudumisha amani ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kuzalisha zaidi katika shughuli zao za kiuchumi ikiwa ni sehemu ya kujiletea maendeleo.

Akizungumza na wananchi wakati wa mkutano wa hadhara ulioitishwa kwa ajili ya kusikiliza kero mbalimbali katika kijiji cha Muluseni, kilichopo Kata ya Ngoma, Ngubiagai alisema, ni wajibu wa kila mwanachi kudumisha amani kwenye eneo lake.

“Tunaelekea kipindi cha Uchaguzi Mkuu ambao utahusisha kuchagua madiwani, wabunge na Rais; kila mmoja ana uhuru wa kumchagua anaemtaka, muangalie waadilifu na wachapa kazi, mshindane kwa hoja na tutambue kuwa kuna maisha baada ya uchaguzi..”

Amewataka wananchi wa Ukerewe kuwa makini na viashiria vyovyote hatarishi vinavyoweza kudhoofisha amani iliyopo na kutoa taarifa haraka kwa vyombo ulinzi na usalama.

Aidha, amewataka wazazi kuacha tabia za kutelekeza watoto na kuwalea katika misingi bora ya upendo ikiwa ni sehemu ya kupunguza matukio ya ukatili yanayoendelea ndani ya jamii.

Nae Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe Dkt.Charles Mkombe alifafanua umuhimu wa watoto kupata chakula shuleni na kuwataka wazazi na walezi kuona umuhimu wa kuchangia huduma hiyo kwa ajili ya ukuaji bora watoto wao.

Sophia Masato, mkazi wa kijiji cha Muluseni alipongeza juhudi za Serikali kwa kuwajali wananchi wake kwa kuwatembelea na kusikiliza kero zao. “Inatia moyo kwa kweli, hata kama itachukua muda angalau wametusikiliza.”

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here